Bunge la Tanzania lataka wataalamu wa afya wanaojituma watunukiwe, wasiingiliwe

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Janeth Masaburi akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Wizar ya Afya, Maendeloe ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamewataka  wanasiasa kuacha kuingilia kazi za kitaaluma zinazotolewa na madaktari pamoja na manesi na badala yake waachwe wafanye kazi zao za kitaaluma kwa uhuru.

Dodoma. Kutokana na matukio kadhaa ya viongozi wa kisiasa kutoelewana na madaktari, Bunge la Tanzania limeshauri iandaliwe tuzo ya madaktari wanaojituma zaidi katika kuwahudumia wananchi na wasiingiliwe katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akichangia mjadala wa bajeti ya wizara ya afya jana Jumanne Mei 7, Mbunge Viti Maalum (CCM), Janeth Masaburi liishauri wizara hiyo kuandaa utaratibu wa kuwatunuku madaktari ili kuwaongezea ari ya utendaji kazi.

“Kuna madaktari wanafanya kazi iliyotukuka, kuna manesi pia, naomba wizara iandae utaratibu wa kuzitambua juhudi zao kwa kuwapa zawadi. Waziri Ummy (Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya) naomba uliangalie hili,” alisema Masaburi.

Wakati Masaburi akisema hayo, kambi rasmi ya upinzani imetahadharisha ongezeko la viongozi wa kisiasa hasa kutoka chama tawala kuingilia majukumu ya wataalamu hao kwamba kuna punguza morali yao ya kazi hivyo kuzorotesha huduma kwa wananchi.

Akisoma hotuba ya kambi hiyo, Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema: “Kumekuwa na mwendelezo wa matukio yanayodhalilisha taaluma ya afya na kuishushia thamani Serikali na kuzipoka mamlaka husika wajibu wake.”

Matiko amekumbusha kuhusu msimamo wa Chama cha Madaktari Tanzania uliotolewa Machi 2017 dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai aliyemtia mbaroni mganga mkuu wa wilaya hiyo, mkuu wa mkoa wa Singida kumuweka ndani mganga mkuu wa wilaya ya Singida na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kumtaka mganga mkuu wa wilaya ya Monduli kutoa maelezo ya malimbikizo.

Hotuba hiyo pia ilitaja tukio la mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi kumsimamisha kazi mganga mkuu wa kituo cha afya Ukami kwa madai ya kudhalilisha wananchi na sakata la kutokukutwa kazini kwa mganga mkuu wa kituo cha afya Ngarenaro kutolewa uamuzi na katibu mwenezi wa CCM kata ya Levelosi.

Kusisitiza hoja hiyo, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema kitendo kilichofanywa na Hapi kimesababisha daktari bingwa aliyedhalilishwa aache kazi na kuondoka hivyo hospitali kukosa huduma zake.

“Mkuu wa mkoa hawezi kumwelekeza daktari bingwa cha kufanya. Serikali iwatie moyo badala ya kuwavunja moyo wataalamu hawa. Itoe mwongozo kuhusu wanasiasa kuwaamrisha madaktari,” alisema Msigwa.