Bunge la Uingereza lakataa mpango wa Serikali

Spika John Bercow 

Muktasari:

London,Uingereza. Wabunge wa Uingereza wamekataa makubaliano ya Waziri Mkuu Theresa May na Umoja wa Ulaya kuhusu Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo, jambo lililouvuruga mchakato wa Brexit.

London,Uingereza. Wabunge wa Uingereza wamekataa makubaliano ya Serikali na Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo, jambo lililouvuruga mchakato wa Brexit.

Hatua hiyo ilisababisha kura isiyokuwa na imani kuwasilishwa, hatua ambayo inaweza kuiangusha Serikali ya Uingereza. Wabunge walioyapinga makubaliano hayo ni 432 huku walioyaunga mkono wakiwa 202 pekee.

Kushindwa huko kwa Serikali kulitarajiwa na wengi ingawa kiasi cha kura alizoshindwa nazo ni jambo ambalo limeuharibu uongozi wake.

Kushindwa huku ni kwa kihistoria kwa kuwa ndiyo mara ya kwanza kwa Serikali kushindwa kwa kiasi kikubwa cha kura katika bunge la nchi hiyo na kunafuatia msukosuko wa kisiasa wa zaidi ya miaka miwili ambapo Waziri Mkuu Theresa May alijiwekea hadhi ya kisiasa kwa kuhakikisha amepata makubaliano ya Brexit.

Muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa na Spika John Bercow Waziri Mkuu May, alizungumza.

"Ahsante Spika.  Spika bunge limeshasema na Serikali itasikiliza. Ni wazi kwamba bunge haliungi mkono makubaliano haya ila kura ya usiku wa leo(juzi) haituambii bunge linaunga mkono hasa kitu gani, haituambii chochote kuhusu ni vipi au hata ikiwa linaunga mkono uamuzi wa Waingereza katika kura ya maoni iliyoamuliwa na bunge hili.

Na watu hasa raia wa Umoja wa Ulaya ambao wamefanya makao yao hapa na raia wa Uingereza wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya, wanastahili kupata uwazi kuhusiana na maswali haya haraka iwezekenavyo," alisema May.

Wananchi wafurahia

Raia wa Uingereza wanaounga mkono kusalia kwenye Umoja wa Ulaya walikuwa wakifuatilia matokeo yaliyoonyeshwa kwenye televisheni zilizokuwa nje ya bunge na wamefurahia kuangushwa kwa makubaliano hayo ya May.

"Nina furaha kwamba makubaliano yameangushwa. Lakini ni hatua ya kwanza tu. Tunachohitaji kwa sasa ni kura nyingine ya maoni. Katika kampeni iliyopita watu walidanganywa, nafikiri kwa sasa sote tunafahamu vyema na ni wakati wa kupata nafasi nyingine ya kupiga kura."

Wasomi nchini

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Anasema: Hapa kuna mambo mawili,  kwanza ni kwamba kujitoa haikuwa jambo la jambo la busara ilikuwa  jazba bila kuangalia maslahi mapana ya wananchi.

Katika dunia ya sasa ushirikiano ni muhimu hata sisi Afrika tunalilia Umoja wa Mataifa wa nchi za Afrka.

Ukiangalia hata Marekani kuna mataifa yao wanashirikiana hata mataifa ya Ulaya wanashirikiana sasa kwanini Uingereza wajitoe?.

Lakini pia kwa kitendo cha kukataa uamuzi  ni kuonyesha kuwa bunge lipo huru.

Kwa hiyo inatakiwa mabunge yetu ya Afrika kama hapa Tanzania tuige, kwamba bunge kama muhimili linatakiwa kuwa huru,na kila mhimili unatakiwa kuwa huru.

Wabunge kuwa huru inatoa nafasi ya kuangalia zaidi maslahi ya wananchi wanaowawakilisha na kufanya  maamuzi bora zaidi kwa taifa.

Mfano hapa Tanzania bunge halipo huru na ndiyo maana limekanganyika sana na tamko lililotolewa na CAG kuwa bunge ni dhaifu walikuja juu kwa sababu ukweli unauma.

Lakini ukweli bunge letu halipo huru, kwahiyo wajifunze kwa wabunge wa Uingereza maana kitendo cha kupingana na Waziri Mkuu, kupingana na Serikali kwa maslahi ya taifa ni mfano wa kuigwa.

Profesa Benson Bana wa UDSM , alisema Hapa ukianza tangu mwanzo katika mchakato utaona kuna msuguano mkali kwani asilimia 52 walikubali lakini 48 walikataa, kwa hiyo ukiangalia wapo ambao hawakukubaliana na huo mchakato.

Wengine hawakuweza kukubaliana kwa  kwa kuwa kujitoa sawa wanaweza wakajitoa lakini kwa taratibu zipi na makubaliano yapi hilo ndilo waliloligomea.

Lakini ukiangalia katika mchakato huu utaona demokrasia inavyofanya kazi kwani waliowengi hawajaridhika na hizo taraibu za kujitoa. Bunge la Tanzania lijijifunze kujenga hoja bila kufuata mihemko ya kisiasa na wajali maslahi ya wananchi.