MUUNGANO WA TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: CIA ilivyoanza kuingilia siasa za Zanzibar -3

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona jinsi Tanganyika na Zanzibar zilivyopitia matukio kadhaa, ikiwamo manowari ya Marekani kuonekana pwani ya Afrika Mashariki na kuzinduliwa kwa gazeti la The Nationalist lililohubiri umoja wa Afrika Mashariki. Tuliishia na mahojiano ambayo yalimfanya balozi wa Marekani aweke bayana kile alichokuwa akifikiria. Sasa endelea...

Katika mahojiano yaliyonukuliwa na kitabu cha Mwalimu: The Influence of Nyerere © 1995, balozi mdogo wa Marekani visiwani Zanzibar, Frank Carlucci alisema kile kilichokuwa akilini mwake, kuwa Marekani pia ilitamani Zanzibar na Tanganyika ziungane, lakini haikujua ifanyaje.

“Nyerere alilazimika kufanya jambo fulani kuhusu Zanzibar. Sijui kwa hakika kama wazo (la Muungano) lilikuwa lake mwenyewe, au kama ni sisi (Wamarekani) tulimpa maagizo,” Carlucci ananukuliwa katika kitabu hicho.

“Hatujui kama kitendo chetu cha kumsukuma afanye lolote kuhusu Zanzibar kilisababisha matokeo yoyote kwake. Natambua kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar ilikuwa ikizidi kuzorota. Kama Tanganyika haingefanya lolote, sehemu hiyo (Zanzibar) ingedhibitiwa moja kwa moja na Wakomunisti.”

Lakini Nyerere alisema yeye ndiye aliyetoa wazo la Muungano kwa Abeid Karume wakati Karume alipomtembelea mjini Dar es Salaam kuzungumzia suala la Okello. Kulingana na maneno ya Nyerere mwenyewe, Karume alikubaliana naye mara moja kisha akapendekeza Nyerere awe Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Ingawa Mwalimu Nyerere alisema yeye ndiye aliyempa Karume wazo la Muungano, hakusema alilipata kutoka wapi na kwa nani, wala hakusema kama alimuita Karume aje Dar es Salaam ili ampe wazo hilo au hali hiyo ilitokea tu katika mazungumzo walipokutana Dar es Salaam.

Katika salamu zake za mwaka mpya kwa wananchi alizotoa Jumatatu ya Januari 2, 1965, Nyerere alidokeza kwamba hata kama ASP ingeingia madarakani kwa njia ya kikatiba na wala si kwa mapinduzi, bado Muungano wa Tanganyika-Zanzibar ungefanyika.

Lakini, kitabu cha Mwalimu: The Influence of Nyerere, kinasema “utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba kulikuwa na shinikizo kubwa la nchi za Magharibi, hususan kutoka Marekani,” kwa Muungano kufanyika kwa hofu kwamba ingesababisha hofu ya ukomunisti katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ingawa kitabu hicho hakikudokeza mambo mengi, uchunguzi wa historia pamoja na marejeo mengi ya Tanzania na nje unaonyesha hali tofauti na jinsi historia rasmi ya Tanzania inavyosema kuhusu Muungano.

Nyerere alipata lini wazo la Tanganyika na Zanzibar kuungana? Na alilipata kutoka kwa nani? Na kwanini? Mbali na maslahi ya Marekani na Waingereza katika Zanzibar, kulikuwa na umuhimu, ulazima na faida gani kwa Tanganyika kuungana na Zanzibar? Je, Tanganyika haingeendelea kuwa nchi ikiwa hakungekuwa na Muungano?

Katika miezi miwili ya maana kwa watu wa Zanzibar (Machi na Aprili 1964), Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilikuwa likifanya bidii kubwa kutengeneza mazingira mazuri ya kufanikisha Muungano. Machoni pa CIA na Waingereza, aliyekuwa na uwezo wa kufanikisha kazi hiyo vizuri zaidi ni Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.

Kwanza, balozi wa Marekani nchini, William Leonhart aliuza wazo hilo kwa Kambona, ambaye naye alilipeleka kwa Nyerere ambaye hakulipokea haraka mpaka alipolitafakari kwa kina (Kambona alianza kushawishiwa tangu akiwa mkutanoni mjini Nairobi—mkutano wa wakuu wa nchi zote tatu za Afrika Mashariki).

Ushawishi huo ulifanyika wiki moja tu kabla ya Aprili 26, 1964, tarehe inayojulikana kama siku ambayo Muungano wa Tanzania ulifanyika. Haijulikani kama Nyerere mwenyewe aliona kama wazo hilo lilifaa au halikufaa. Lakini mara baada ya kulipokea kutoka kwa Kambona, hakuona kama lilikuwa la maana sana kwa sababu badala ya kukaa na Kambona kulijadili, alimpangia Kambona ziara ya mikoani.

Wazo hilo lilipokubaliwa, mbinu ya kwanza iliyotumiwa na CIA katika kujenga Muungano huo ni kuwagombanisha wanamapinduzi wa Zanzibar na mbinu ya pili ikawa ni kuwaaminisha viongozi wa Tanganyika na Zanzibar kwamba kulikuwa na tishio la ukomunisti lililokuwa likienea na kwamba watu waliokuwa hatarini zaidi ni viongozi wa Tanganyika na Zanzibar na serikali zao. Isitoshe waliosaidia kuzima maasi, na ambao wangeyazima tena baadaye ikiwa yangetokea, ni mataifa ya Magharibi.

Hata kabla wazo hilo halijafikishwa kwa viongozi (wa Tanganyika na kisha wa Zanzibar), Marekani, kwa kuitumia CIA na kwa kiasi fulani Uingereza, walianza kufanya kazi mapema tangu siku ya mapinduzi ya Unguja, yaani Januari 12 na, huenda, walikuwa tayari wameanza kufanya kazi mapema zaidi hata kabla ya mapinduzi.

Ziko nadharia zinazosema kuwa huenda wao ndio walioruhusu au kulinda kufanyika kwa mapinduzi hayo. Hali hii inaeleza ni kwanini alitumwa mtu maalumu, kwa mwamvuli wa ubalozi, lakini jasusi wa Marekani, kwenda Zanzibar kuendesha mambo kwa jinsi walivyotaka wao.

Kulikuwa na mtandao uliotengenezwa vyema ulioandaliwa na kutumiwa na wataalamu wa CIA. Baada ya kuona kuwa CIA ina uwezo wa kuzitawala siasa za Afrika Mashariki, ndipo mabalozi walianza kuhusishwa au kuhusika kikamilifu katika mtandao huo.

Machi 6, 1964, katika mfululizo wa habari zilizokuwa zikipelekwa kwa simu (telegrams) kutoka Washington, Marekani, David Dean Rusk, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa wakati ule, alituma ujumbe ofisi za ubalozi za Marekani za Dar es Salaam na Nairobi akizisisitiza balozi hizo, pamoja na mambo mengine, “kuwafuata Nyerere na Kenyatta na Obote haraka iwezekanavyo kuwaeleza hatari iliyopo kwa Karume kumkumbatia Babu na kuwaomba waingilie kati jambo hilo ili wamueleweshe Karume kujua hatari inayoweza kusababishwa na Babu kwa cheo cha Karume na usalama wa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa ujumla”.

Wamarekani walimchukia Babu kwa sababu ya ukomunisti wake na pia mwanasiasa huyo msomi kutowapenda Wamarekani na pande zote zilijua hilo.

Kwa hiyo Wamarekani walijua ilikuwa vigumu kwa Babu kubadilisha msimamo wake na hivyo kuandaa mbinu za kummaliza kisiasa.

Itaendelea kesho