DC Hai awaondoa ukumbini mkurugenzi, mwenyekiti wa halmashauri

Muktasari:

  • Uamuzi wa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuwaondoa ukumbini mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri hiyo waliokuwa wakiongoza kikao cha kamati ya fedha umezua taharuki kwa viongozi hao

Hai. Uamuzi wa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuwaondoa ukumbini mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri ya Hai waliokuwa wakiongoza kikao cha kamati ya fedha umezua taharuki kwa viongozi hao.

Mkurugenzi huyo, Yohana Sintoo na  mwenyekiti, Helga Mchomvu  na wajumbe wengine waliondolewa katika ukumbi huo huku mkuu huyo wa wilaya akiingia na watu wengine kwa ajili ya kutumia ukumbi huo.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo jioni Jumanne Januari 15, 2019, Sabaya amesema aliwaondoa akiwataka kutumia ukumbi mwingine.

Amesema kikao hicho kilikuwa na wajumbe 10, aliwataka  kuhamia ukumbi mdogo ili yeye ahudumie zaidi ya wamachinga 200 walioomba ukumbi huo mkubwa mapema.

Akisimulia tukio hilo leo,  Mchomvu amesema kitendo hicho hakipaswi kufanywa na kiongozi huyo wa Serikali.

“Tulikuwa na kikao cha kamati ya fedha katika ukumbi wa Halmashauri. Tumeanza tangu saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana.  Aliingia  mkuu wa wilaya na kututaka kutoka nje ya ukumbi na kuamuru waliokuwa naye nje ya ukumbi huo, kuingia ndani,” amesema.

“Kikao chetu kilikuwa halali na ni cha kisheria. Aliwanyanyua watu wote tuliokuwepo katika kikao, akiwemo mkurugenzi, wakuu wa idara.”

Ameongeza, “Eneo lile lina kumbi nyingi ambazo angeweza kuzitumia lakini amevunja kikao cha kamati ya fedha kilichokuwa kinaendelea.”

Amesema kuvunjwa kwa kikao hicho kutasababisha baadhi ya mambo kukwama.