Dar yapata Sh220 bilioni kukabili mafuriko Jangwani

Dar es salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema Serikali imefanikiwa kupata dola 100 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh220 bilioni za Kitanzania) kwa ajili ya kumaliza tatizo sugu la mafuriko katika bonde la Mto Msimbazi.

Makonda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanahabari eneo la Jangwani ambako alifanya ziara ya kukagua athari za mvua zilizonyesha mfululizo kwa zaidi ya wiki.

Alisema wataalamu wa maafa wa ofisi yake wamepiga picha eneo linalozungukwa na Mto Msimbazi kwa kupata taswira halisi itakayowezesha kupata mkakati wa kuikabili changamoto ya mafuriko katika makazi.

Bonde la mto huo linalohusisha daraja la Jangwani, lilikuwa likitumika kwa shughuli za michezo kabla ya wananchi kuanza kujenga pembeni. Eneo hilo pia ndilo lina karakana ya waendeshaji mradi wa mabasi yaendayo kasi, Udart, ambayo hufurika maji kila wakati wa mvua kubwa na kusababisha mabasi kuharibika.

Makonda alisema Serikali imepata fedha hizo za mkopo kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuijenga upya Jangwani na tayari upembuzi yakinifu umeanza na utakamilika mwezi ujao.

”Lengo iwe ni mwisho wa changamoto kubwa tulizozoea kuziona. Design (mchoro) inayoandaliwa ni ya kuhimili hayo maji ili yaende baharini,” alisema Makonda.

Wakati Makonda akieleza hayo, kaimu mkurungenzi wa mradi wa mabasi hayo (Dart), Ronald Rwakatale alisema tayari wameshaanza kuangalia maeneo kwa ajili ya kuhamishia karakana hiyo, ikiwamo eneo la Ubungo ambako kuna kituo cha mabasi yaendayo nje ya Dar es Salaam.

“Hata leo tulikuwa na kikao na Tamisemi kuhusu Mradi ya Uendelezaji wa Jiji (DMDP), kwa hiyo tunajipanga,” alisema.

Katika ziara hiyo alikuwepo mbunge wa zamani wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, ambaye alishauri utekelezaji wa mradi huo ufanyike sambamba na kuondoa makazi yaliyofunga maeneo ya kupumlia mto huo, kama kuhamisha wakazi wa Kigogo Sambusa na hata kuondolewa kwa kituo cha mwendokasi.

Shule zilizoathiriwa na mvua

Katika hatua nyingine, viongozi wa manispaa za jiji wameiambia Mwananchi kuwa hatua mbalimbali zinaendelea kukarabati madarasa na vyoo vya shule vilivyoathiriwa na mvua.

Mkurugenzi wa Ilala, Jumanne Shauri alisema manispaa yake itatumia takribani Sh60 milioni kwa ajili ya ukarabati katika shule nne za msingi. Alisema shule ya Kiboga, Mwale imebomoka ukuta wa madarasa manne na choo kimoja sawa na vyoo vya shule za Majani ya Chai na Chanika.

Mkurugenzi wa Kinondoni, Aaron Kagurumjuli alisema manispaa yake itatumia Sh90 milioni kukarabati vyoo katika shule za msingi za Hananasif na Bunju A huku ikiandaa bajeti nyingine ya kujenga ukuta wa madarasa ya shule ya Msingi Tandale.

Juzi Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo Manispaa ya Temeke iliathiriwa na mafuriko hayo na kusababisha masomo kusitishwa kwa muda.