Diwani Chadema asimulia alivyowekwa ndani na RC Mara akidaiwa kukunja nne kikaoni

Muktasari:

Diwani wa Susuni (Chadema), Abiud Solomon amesimulia jinsi alivyoondolewa kwenye kikao na mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima na kuwekwa ndani kwa saa saba kwa sababu alikunja nne kikaoni


Tarime. Diwani wa Susuni (Chadema), Abiud Solomon amesimulia jinsi alivyoondolewa kwenye kikao na mkuu wa mkoa wa Mara,  Adam Malima na kuwekwa ndani kwa saa saba kisha kuachiwa akielezwa kuwa ana dharau kwa kuwa alikunja nne kikaoni.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 2, 2019 amesema Malima alitoa agizo hilo kwa polisi kumweka ndani kwa madai kuwa ameonyesha dharau kwenye kikao cha kumtambulisha mkuu mpya wa wilaya ya Tarime, Charles Kabeho.

Katika tukio hilo lililotokea jana Ijumaa Februari Mosi, 2019, Solomon amesema kabla ya kuondolewa alihojiwa kuhusu wadhifa wake, “lakini nilishangaa kusikia agizo la kuniweka ndani kisa nimekunja nne kwenye kikao cha mkuu wa mkoa.”

“Niliwekwa ndani kuanzia saa saa 9 alasiri hadi saa 3 usiku baada ya  viongozi wangu wa chama kufanya taratibu za kuniwekea dhamana wakafanikiwa kunitoa lakini nikatakiwa kurudi siku ya Jumatatu Februari 4.”

Ameongeza, “Tulikuwa na kikao cha kumkaribisha mkuu wa wilaya mpya, nilipata nafasi ya kukaa eneo la waandishi wa habari ili kuwapisha wapite, nililazimika kubebanisha miguu yangu (kukunja nne)  ili kutoa nafasi ya wao kupita na kufanya kazi yao vizuri, ila ikachukuliwa kwamba namdharau mkuu wa mkoa.”