Dk Bashiru adai CCM imewakataa wabunge watatu wa upinzani

Thursday July 11 2019

Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally akisalimiana

Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally akisalimiana na mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya wakati wa mapokezi yake kwenye ziara ya siku moja Wilayani Simanjiro leo. Picha na Joseph Lyimo 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Mirerani. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho tawala nchini kimewakataa wabunge watatu wa vyama vya upinzani walioomba kujiunga nacho.

Amesema waliwakataa baada ya kubaini hawawezi kukidhi vigezo vya kuwa wabunge wa CCM.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 11, 2019 katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara wakati akizungumza katika uwanja wa Barafu katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani humo.

Amesema kabla ya mbunge kujiuzulu na kujiunga na CCM wanakubaliana na kuwahoji mambo mengi ikiwemo dhamira zao na watakayoyafanya kwa ajili ya wananchi.

Amebainisha kuwa CCM si chama cha kuchukua kila mtu na ndio sababu wamewakataa wabunge hao, akijitamba kuwa kama wangewapokea, upinzani ungekwisha.

Hata hivyo, amewapongeza wabunge wawili wa Mkoa wa Manyara waliokuwa Chadema na kuhamia CCM ambako walipitishwa kuwania tena ubunge na kushinda.

Advertisement

Wabunge hao ni James Ole Millya wa Simanjiro na Pauline Gekul wa Babati Mjini, akibainisha kuwa ni viongozi makini.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Simon Lulu amesema majimbo yote saba ya Mkoa huo yanaongozwa na wabunge wa CCM.

Advertisement