Dk Bashiru asema Magufuli atang’atuka urais

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema muda ukifika Rais John Magufuli atang’atuka madarakani kama ilivyokuwa kwa marais wengine wastaafu

 

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema muda ukifika Rais John Magufuli atang’atuka madarakani kama ilivyokuwa kwa marais wengine wastaafu.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 23, 2019 katika uzinduzi wa Mkakati wa Kukomaza Demokrasia kwenye ngazi ya mashina ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dodoma.

“Yupo mwingine hapa, hapana usifanye hivyo si msimamo wa  CCM. Hatutaki kuwa na viongozi masultani ndani ya CCM ama ndani ya Serikali ya CCM ama ndani ya CCM yenyewe,” amesema Dk Bashiru.

Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia ni miongoni mwa wanachama wa CCM ambao mara kadhaa wamekuwa wakitoa mapendekezo kutaka Rais Magufuli kuendelea kubaki madarakani licha ya Katiba kueleza kuwa kipindi cha rais kukaa madarakani ni miaka 10.

Katika mkutano huo wakati Dk Bashiru akieleza hayo Nkamia ambaye pia alikuwepo alisimama.

“Dk John Magufuli atamaliza awamu yake ya kwanza ya miaka mitano na ataomba ridhaa ndani ya chama chake kwa kufuata Katiba. Nina uhakika kuwa mtampa kura nyingi za kutosha,” amesema.

Amesema atafanya hivyo kama ilivyokuwa kwa Julius Nyerere na maraisi wengine na kwamba watampata Rais bora baada ya Magufuli kumaliza kipindi cha uongozi.

“Napenda kuhitimisha mjadala usio rasmi unaoendelea kuhusu hatma ya nchi hii baada ya John Pombe Magufuli. Hatma ya nchi hii iko mikononi mwa wana CCM,” amesema Dk Bashiru.