Dk Bashiru asema RC Mwanza hatohamishwa, ataja sababu

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  John Mongella hataondolewa  mkoani humo hadi wakamilishe kazi ya kuufanya kuwa Mkoa ambao wananchi wake watajitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mwanza.  Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  John Mongella hataondolewa  mkoani humo hadi wakamilishe kazi ya kuufanya kuwa Mkoa ambao wananchi wake watajitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Mongella anafanya kazi nzuri na ni moja ya viongozi wanaochapa kazi, mfano halisi ni pale ilipotokea ajali ya Mv Nyerere (iliyozama), alionyesha dhahiri utendaji wake, " amesema Bashiru.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 3, 2019 mkoani Mwanza wakati akizungumza na seneti ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.

Amesema maneno yanayozungumzwa kuwa mkuu huyo wa Mkoa atagombea ubunge Wilaya ya Ilemela si ya kweli, amemhakikishia kufanya naye kazi pamoja.

"Waliokuwa wanamsingizia kuwa ataenda kugombea ubunge haendi huko na akiwa king'ang'anizi atakosa vyote ubunge na ukuu wa Mkoa, " amesema Bashiru.

Amewataka viongozi wengine kushirikiana pamoja kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 ili kupata viongozi bora.