Dk Tizeba atoa mbinu ya kupata soko la nyama nje ya Tanzania

Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba

Muktasari:

Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba amesema nyama ya Tanzania haipati soko nje ya nchi kwasababu si eneo huru la magonjwa ya mifugo.

Dodoma. Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba ameitaka Serikali kutoa chanjo ya mifugo kwa lazima kama inataka kuwa eneo huru la magonjwa na hivyo kupata soko la nyama nje ya nchi.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2019/20 bungeni leo Jumanne Mei 21 2019, Dk Tizeba amesema suala la mazao ya mifugo haliishii kwenye kujenga viwanda.

Amesema hiyo inatokana hata na mazao machache yaliyopo yanakabiliwa na changamoto ya soko kwasababu eneo kubwa la ufugaji halijawa huru na magonjwa.

“ Sababu ya homa ya mapafu na ile ya East coast fever yanazuia uuzwaji wa nje wa nyama ya Tanzania na namna pekee ya kuondokana na hiki kikwazo ni kwa kufanya chanjo ya lazima,” amesema.

Amesema utaratibu wa kuwaambia wafugaji wachanje kwa hiari ndiyo inayofanya nchi kushindwa kuondokana na kikwazo hicho.

“Leo jumuiya nzima ya Ulaya haipokei nyama kutoka Tanzania, Marekani haipokei nyama kutoka Tanzania na huko ndiko kwenye soko lenye bei kubwa,” amesema.

Dk Tizeba amesema suala la uvuvi umekuwa kizunguzungu na kwamba yeye alifanya marekebisho makubwa ya kanuni.

Hata hivyo,  baadhi yametekelezwa lakini marekebisho katika Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambayo ina mwaka mmoja bado haijaingiza fedha.

“Tumetunga sheria na kanuni ili ituongezee mapato ama ipoteze mapato. Naiomba Serikali  jambo hili lifanyiwe tafakari,” amesema.

Amesema dhahabu haifanani na dhahabu, usipoichimba itabaki katika shimo husika bali wanatembea na kwenda maeneo mengine.

Amesema mrabaha wa asilimia 0.4 kwa kila kilo ya samaki ulikataliwa na jambo hilo liliwafanya kukaa miezi minane bila kutoa leseni .

Dk Tizeba amesema waliamua kugawa jambo hilo yaani miezi sita walipe na miezi sita wasilipe, walikuja wavuvi 51.

Amesema jambo hilo lisipoangaliwa, mapato ya samaki yanazidi kupotea.

Amesema katika nchi za Kenya na Djbout zipo meli zaidi ya 300 zinasubiri samaki wapitie katika eneo lao wavue, lakini Tanzania bado inasubiri ushuru wa asilimia 0.4 kwa kilo moja ya samaki ili tupate mrahaba.