Dudu Baya aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Jeshi la Polisi limemuachia kwa dhamana msanii Dudu Baya baada ya kumshikilia kwa saa kadhaa katika kituo cha Polisi Oysterbay


Dar es Salaam. Hatimaye Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limemuachia kwa dhamana msanii wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini maarufu kwa jina la Dudu Baya, baada ya kumshilikia kwa saa kadhaa.

Dudu Baya alikamatwa juzi Jumatano, Februari 27 usiku nyumbani kwake Mbezi na kufikishwa katika kituo cha Polisi Oystebay kwa ajili ya mahojiano.

Hatua hiyo ilikuja  baada ya Waziri wa Habari na Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuagiza Jeshi la Polisi na Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) kumchukulia hatua mwanamuziki huyo kwa makosa ya kumdhihaki, aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Akizungumza na Mwananchi leo, Ijumaa Machine 1, 2019, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mussa Taibu amesema walimwachia msanii huyo jana Alhamisi, Februari 28 saa 9:00 mchana baada ya kumaliza kumuhoji.

Kamanda Taibu amesema pamoja na kumuachia huko bado upelelezi unaendelea dhidi yake.

Kamanda huyo alipotakiwa kusema ni lini hasa msanii huyo atapaswa kurudi tena kituoni hapo, amesema suala hilo ameiachia ofisi ya upelelezi na kuahidi kulitolea majibu badaye.

"Unajua kwa sasa jambo hili lipo katika ofisi ya upelelezi wao ndio wanajua ni lini wamempangia arudi, ila ninachojua ni kwamba upelelezi dhidi ya msanii huyo unaendelea," amesema Kamanda Taibu.

Dudu Baya alikamatwa na polisi na kufunguliwa jalada la kesi lenye namba OB/RB/2029/2019 la matumizi mabaya ya mitandao kutokana na kitendo chake hicho cha mara kadha kumkashifu marehemu Ruge kabla na baada ya kufariki kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kujirekodi video kwa nyakati tofauti.