Gharama za kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu

Thursday February 7 2019

 

Benki zimeanza kufanya vizuri sasa hivi na zinaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha zinatengeneza faida. Wakati taasisi hizi zikitekeleza mikakati yao, wateja wanapaswa kuwa makini zaidi kwenye miamala yao kwani gharama zimepanda.Mwaka 2014, sekta ya benki na taasisi za fedha ilipata jumla ya faida ya Sh426 bilioni ambayo ilipanda mpaka Sh438 bilioni mwaka 2015 halafu ikashuka hadi Sh423 bilioni mwaka 2016 na Sh286 bilioni mwaka 2017.Baada ya kushuka kwa faida kwa miaka miwili mfululizo, mambo yameanza kubadilika mwaka jana. Kwa mujibu wa taarifa za fedha zilizochap-ishwa na taasisi hizo kwa robo ya mwisho ya mwaka 2018, nyingi ama zimeondoka kwenye hasara na kupata faida au zimeendelea kupata faida kubwa zaidi huku zikipunguza kiasi cha mikpo isiyolipika.Kuhakikisha ufanisi huo unaendelea mwaka huu, benki nyingi zimeanza kupandisha ghara-ma za miamala tofauti inayofanywa na wateja. Hili linatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali ya huduma za benki. Kwa wateja wa taasisi hizi, huu ni wakati wa kuwa makini zaidi ili akiba iliyopo isiishie kugharamia miamala ya benki badala ya kufanikisha mambo mengine.Gharama mpyaKitu muhimu unachopaswa kuzingatia ni idadi ya miamala unayofanya kwa siku, wiki au mwezi ambayo ni   msingi wa mapato ya benki kwa sasa.

Baada ya kuijua miamala unayofanya, ni vyema ukafahamu kila kila sehemu unayopata huduma uitakayo ina tozo tofauti. Gharama za kutoa fedha ndani ya benki kwa mfano, ni tofauti na kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM) au kuhamishia kwenye simu yako ya mkononi.

Mabadiliko ya gharama hizo yamefanywa pia na benki kubwa zinazohudumia wananchi wengi zaidi nchini ambazo ni CRDB, NMB na NBC. Kati ya asilimia 16.9 ya Watanzania wanaotumia huduma za benki, asilimia 40 kati yao wanazipata kutoka benki hizi tatu.

Benki ya CRDB imepandisha gharama za kuangalia salio, kutoa au kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu.

Awali wateja wa benki hiyo walikuwa wakilipa Sh944 kutoa fedha kwenye ATM lakini sasa imeongezeka hadi Sh1,200 kwa wateja waliopo nchini lakini watakaokuwa nje ya mipaka ya Tanzania watalazimika kulipa Sh8,000.bo yatakayochangia kukua tena kwa utalii.

Ukitaka kujua salio ukiwa ndani ya tawi la Benki ya CRDB basi utalipa Sh2,000 na ukiwa nje ya nchi ni Sh1,180. Tozo ya kutoa fedha kwenye ATM ni kubwa nchini kuliko ukiwa umesafiri kwenda ughaibuni.

Kwa wateja wa NMB watakaotoa fedha kwenye ATM watatozwa Sh1,150 tofauti na Sh944 ya awali huku kutoa fedha ndani ya tawi ikiwa Sh6,500 kutoka Sh4,012 ya awali na kuuliza salio kaunta Sh2,300.

Kwa wateja wa NBC, kuuliza salio kaunta ni gharama kubwa kuliko kufanya hivyo kwenye ATM.

Wakati NBC na CRDB zikitoza kuuliza salio kaunta, huduma hiyo kwa wateja wa Benki ya NBC ni bure watatozwa Sh4,130 wakitaka kutoa fedha ndani watakapohitaji hadi Sh20 milioni lakini kwa kiwango zaidi ya hapo watakatwa asilimia 0.12 ya kiasi wanachotoa ila isizidi Sh200,000. Awali, benki hiyo ilikuwa inatoza Sh3,000 kutoa fedha ndani.

Gharama za kuuliza salio kwenye ATM za NBC zimeongezeka hadi Sh400 kutoka Sh354 na Sh600 kutoka Sh590 kwa ATM za benki nyingine.

Watakaotaka kutoa fedha kwenye ATM watalipia Sh1,200 tofauti na Sh1,180 ya zamani.

Huduma kwa simu

Wateja wa Simbanking ya CRDB sasa watalipa Sh400 kujua salio kutoka Sh354 na watatozwa Sh699 wakitaka kuhamisha fedha kwenda akaunti nyingine.

Wateja hao watalipa kiwango tofauti kutegemea kiasi wanachohamisha kutoka benki kwenda kwenye simu zao. Awali, kuhamisha hadi Sh200,000 ada yake ilikuwa Sh2,499 lakini sasa kuna mabadiliko. Sasa, watakaohamisha kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 watakatwa Sh1,500.

Waliokuwa wanahamisha kati ya Sh500,0001 hadi Sh1 milioni ambao walikuwa wanalipa Sh6,399 wataendelea kulipa kiasi hicho.

Wanaohamisha kiasi kidogo, Sh5,000 watalipa gharama kubwa zaidi, asilimia 30 wakati wale wa kiwango ch ajuu zaidi, Sh1 milioni wakitozwa asilimia 0.64 tu ya kiasi wanachohamisha.

Benki ya NMB, wateja watakaohamisha kati ya Sh1,000 hadi Sh5,000 watatozwa Sh1,000 au Sh3,000 wakihamisha kati ya Sh5,001 hadi Sh30,000. Kwa watakaohamisha kati ya Sh600,001 hadi Sh1 milioni watalipa Sh6,500.

Ukihamisha Sh1,000 utalipa gharama kubwa zaidi, asilimia 100 wakati wanaojiweza zaidi, watakaohamisha Sh1 milioni watatozwa asilimia 0.65 tu.

Wateja wa NBC wataruhusiwa kuangalia salio kwa Sh400 kutoka Sh354 kwakutumia simu zao za mkononi lakini watatozwa Sh3,000 wakihamisha kati ya Sh1,000 hadi Sh100,000 au Sh4,800 kati ya Sh500,001 hadi Sh1 milioni.

Kuhamisha Sh1,000, mteja wa NBC atatakiwa kulipa asilimia 300 au asilimia 0.48 akihamisha Sh1 milioni.

Maoni

Mchumi na mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema benki zinajitahidi kuhakikisha zinaongeza mapato kutoka vyanzo vingine baada ya kushuka kwa riba za mikopo.

“Biashara kubwa ya benki ni kutoa mikopo hivyo riba inaposhuka mapato hupungua pia. benki zetu hazina ubunifu, zinategemea zaidi vyanzo vilevile yaani zikikosa riba zitaongeza gharama za miamala au kamisheni,” anasema Dk Pastory.

Kinachofanyika hivi sasa, anasema ni benki kujitahidi kupunguza gharama za uendeshaji ndio maani zinataka wateja wengi ama watumie simu au ATM ili wahudumu wa ndani nao wawe wachache.

Mtaalamu huyo anazishauri taasisi za fedha kujielekeza vijijini kwenye wananchi wengi zaidi ambako wakiwakopesha watu wengi wataongeza mapato.

“Kupandisha gharama ni kutowahamasisha wananchi kutumia huduma zao. Watu watakosa sababu, hapa Benki Kuu inapaswa kuangalia cha kufanya,” anatahadharisha.

Mmoja wa wateja wa benki kutoka Mbagala jijini Dar es Salaam, Daniel Nzyungu anasema kupanda kwa gharama hizo kunamshangaza.

“Kweli nihamishe Sh5,000 au Sh10,000 kutoka kwenye akaunti kuja kwenye simu halafu nikatwe Sh1,500 au zaidi ya hapo na nikitaka kuitoa nikatwe tena Sh1,200! Inaonekana ni pesa ndogo lakini ikikatwa mara nne inatosha mlo wa familia yangu,” anasema Nzyungu.


Advertisement