Halmashauri zatakiwa kusimamia fedha za afya

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri nchini kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika sekta ya afya

Siha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu katika sekta ya afya.

Ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2019 wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la maabara la Hospitali ya Taifa ya Kifua Kikuu  Kibong'oto wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.

"Halmashauri simamieni vizuri fedha hizi na hakikisheni hazichomolewi ovyo na sisi Serikali kila mwezi tumetenga Sh257milioni kwa ajili ya hospitali za wilaya," amesema Majaliwa.

Awali, mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Riziki Kisonga amesema ujenzi wa maabara hiyo hadi sasa umegharimu Sh3.37bilioni.

"Mpaka jengo hili likamilike linahitaji zaidi ya Sh8.86bilioni, hadi sasa kuna upungufu wa zaidi ya Sh5.6bilioni," amesema Dk Kisonga.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema jengo hilo la maabara lina uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi 700, akibainisha wagonjwa wengi wa kifua kikuu wanatokea katika maeneo ya machimbo ya madini.