Haya ndiyo magari ya umeme yanayoweza kupeleka watalii Mlima Kilimanjaro

Friday July 12 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mlima Kilimanjaro ambao ndio mrefu zaidi kuliko yote Afrika, ni moja ya vivutio vikubwa vinavyoingiza maelfu ya watalii kila mwaka Tanzania.

Mbali na urefu wake, Mlima Kilimanjaro ambao ni fahari ya Tanzania na Afrika kwa ujumla umeendelea kuwa kivutio kwa kubaki katika uasilia wake, mandhari nzuri huku ukizunguukwa na misitu.

Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuboresha utalii nchini ili kuvutia watalii na kuhakikisha idadi ya watembeleaji wa ndani na hata wale wanaotoka mataifa ya kigeni inaongezeka katika vivutio mbalimbali vilivyopo.

Moja ya mikakati iliyokusudiwa kutekelezwa katika kurahisisha na kusogeza huduma kwa watalii ni uanzishwaji wa safari za magari ya umeme yapitayo juu kwa kutumia nyaya (Cable cars) kwenda Mlima Kilimanjaro.

Kwa sasa takribani watalii 50,000 hupanda mlima huo kila mwaka kwa kutumia njia za miguu zinazoweza kumfikisha mtalii katika kilele cha Uhuru au chini ya hapo katika vituo tofauti vilivyowekwa.

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imetangaza kusudio la kutaka kuanzisha usafiri huo wa magari ya umeme yapitayo katika nyaya ili kuwawezesha watalii kupanda Mlima Kilimanjaro au kuutembele na kushuhudia mandhari yake kwa ukaribu zaidi.

Advertisement

Inaamini kwa kuanzisha usafiri huo kwenda Mlima Kilimanjaro utaongeza idadi ya watalii wanaopanda mlima kwa asilimia 50.

Hata hivyo, hatua hiyo hivi karibuni iliibua mjadala kwa mawaziri wawili wenye dhamana tofauti ambao awali walipishana kimtazamo juu ya hatua hiyo kabla ya baadae kufikia mwafaka na kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kila mmoja kuonesha kumwelewa mwenzake.

Mjadala uliibuka kutokana na ujumbe uliotumwa na mwanaharakati Haki Ngowi kupitia akaunti yake ya Twitter aliyeandika Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inatarajia kuanzisha usafiri wa magari ya umeme yanayopita juu katika nyaya kupeleka watalii mlimani.

Baada ya ujumbe huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliandika “Itabidi watu wa mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza klabla hawajaanza na tutafanya tathmini ili kujua matokeo kwa mazingira na mkakati wa kudhibiti.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi kigwangalla naye kupitia Twitter akaandika katika kile kilichotafsiriwa kama alikuwa akimjibu Makamba “hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake? Hizi haziharibu mazingira. Cable car inapita juu inaharibu mazingira gani?”

Mjadala huo ulilenga kila mmoja kusimamia eneo lake kuhakikisha ama hatua hiyo inatekelezwa ili kuongeza kipato au haitekelezwi mpaka pale usama wa mazingira utakapothibitishwa na wataalamu.

Kutokana na mjadala ule ni muhimu kutambua ni kwa kiasi gani cable cars zina umuhimu nchini kwa kuchochea utalii na usafiri, pia kuona athari zake zinazohofiwa kuifika nchi wakati wa maandalizi na utekelezaji wake.

Mhandisi aeleza uzoefu

Mhandisi wa mfumo wa uendeshaji wa vyombo hivyo, Mustafa Madafa kutoka kiwanda cha mbao cha Tembo Chipboard Ltd, kilichopo Mkumbara, Tanga anasema kiwanda chao kimekuwa kikitumia cable cars kwa zaidi ya miaka 50 sasa kwa ajili ya usafirishaji magogo na wakati mwingine watu wanapotekeleza majukumu ya kiwanda.

Anasema kiwanda hicho kinachoendesha shughuli zake kati ya Mombo la Lushoto mkoani Tanga, kilianza kutumia magari hayo tangu mwaka 1970 baada ya kuzinduliwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Madafa anasema magari hayo katika kiwanda hicho yamekuwa yakitumika kusafirisha magogo kutoka msitu wa Lushoto na kuyapeleka kiwandani Mkumbara. “Mara nyingi pia tumekuwa tukisafirisha watu hasa watumishi na wengineo katika eneo hili”. Kwa mujibu wa Madafa, gari hilo linatoa huduma katika eneo lenye umbali wa kilomita mbili ambapo hutumia dakika saba kutoka linapoanzia safari hadi mwisho wakati awali walilazimika kutumia muda mwingi kwa kuzunguuka huku wakitumia mafuta mengi kwenye magari yanayotoa huduma.

“Nimeanza kushughulika na cable cars tangu kipindi hicho, Serikali imenipeleka nje mara kadhaa kwenda kusomea katika nchi mbalimbali ikiwamo Uswiss na Ujerumani ambako wenzetu matumizi ya cable cars ni makubwa zaidi. Naweza kusema hakuna athari kubwa kwa mazingira, bali matumizi ya magari hayo yana faida kiuchumi hasa katika sekta ya utalii na usafirishaji.

“Ukienda katika nchi za wenzetu cable car zinapishana angani kama usafiri wa ardhini, huwezi kusikia madhara makubwa ya ajali bali faida zake ni nyingi mno,” alisema.

“Kama Serikali imekusudia kufanya hivyo kwa ajili ya kuongeza watalii Mlima Kilimanjaro naamini hilo litawezekana na litakuwa na faida nyingi zaidi. Mifano itazamwe Uswis nchi yenye milima mingi ambapo watalii huitembelea kwa cable cars wakitokea hotelini walikofikia,” anasema.

Anasema kiwanda hicho bado kinaendelea kulitumia gari hilo ingawa kwa sasa kimesimama kwa muda baada ya kuchukuliwa na Serikali ikiwa katika mchakato wa kupatikana mwekezaji wa kukiendeleza.

Nchi zinazotumia magari hayo Afrika

Afrika Kusini: ni moja ya nchi zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha usafiri huo na kuchochea utalii.

Magari hayo nchini humo husafirisha maelfu ya watalii kila mwaka kwenye milima ya Table Mountain ambako hupata fursa nzuri ya kuuona mji wa Cape Town kwa kuwa huwa juu ya mlima.

Cable car katika milima hiyo inatumiwa kama chachu ya kuongeza na kushawishi utalii kwani gari hilo linapofika katika kilele cha mlima huzunguuka ili kutoa fursa kwa waliomo ndani kuona pande zote na kupiga picha. Abiria 65 hujaza gari moja na kupelekwa katika kilele cha mlima huo ndani ya dakika tano. Takribani watu milioni 27 wanakadiriwa kupanda magari hayo mpaka sasa kwenda Table Mountain wakiwamo raia wa kigeni wanaokwenda kwa ajili ya utalii.

Nigeria: nayo ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazotumia usafiri huo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kubwa zaidi ikiwa ni kusafirisha watalii.

Cable car zinatumika kusafirisha watu kwenda Mlima Obudu ikikatisha eneo lenye mto la Cross River State.

Mradi huo uliendelezwa mwaka 1951 huku wazo lake likiwa katika makaratasi tangu mwaka 1949.

Baada ya kuendelezwa tangu mwaka 2005, magari ya umeme yapitayo katika nyaya sasa yanafika umbali wa mita 870 (futi 2,850) kutoka pale inapoanzia safari na kutoa fursa kwa watalii kupata picha nzuri wakiwa angani. Magari hayo yanatembea kilomita 110 hadi mji wa Mashariki wa Ogoja karibu na eneo la mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.

Algeria: inatarajia kumia magari ya umeme kuunganisha miji ya Tafoura ulio karibu na bandari ya Algiers na El Biar takribani kilomita saba. Eneo hilo halijaunganishwa na miundombuni ya usafiri wa ardhini kutokana na jografia yake kuzunguukwa na milima. Pia ianatarajiwa kutumia mradi kama huo kuiunganisha miji ya Bab-El Oued na Zghara ambako kunazunguukwa na milima ya Coucou.

Advertisement