Hoteli Arusha yawekeza Sh184 bilioni

Mkuu mkoa Arusha Mrisho Gambo akiwa na meneja mkuu wa hoteli Gran Melia Nicolas Konig baada ya kutembelea hoteli hiyo na kupokewa na wafanyakazi. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amefanya ziara katika hoteli mpya ya Gran Melia iliyowekeza Sh184 bilioni.

Arusha. Sekta ya utalii mkoani Arusha inatarajiwa kuimarika zaidi kutokana na uwekezaji wa Sh184 bilioni wa hoteli ya Gran Melia ambayo itafunguliwa mwezi ujao.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu baada ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama kutembelea hoteli hiyo.

Gambo amesema hoteli hiyo licha ya kusaidia kukuza sekta ya utalii, pia inatarajiwa kutoa ajira za vijana 300 na kulipa kodi za Serikali.

"Huu ni uwekezaji mkubwa ambao Rais John Magufuli amekuwa akihimiza kwani hoteli hii hadi kukamilika itakuwa na vyumba 171 na itatoa huduma kwa viwango vya kimataifa," amesema.

Gambo aliagiza Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha na idara ya kazi kukaa na mwekezaji huyo kutatua changamoto ya ajira kwa wafanyakazi wa kigeni.

Awali meneja wa hoteli hiyo, Nicolas Konig  alisema hoteli hiyo inatarajia kutoa huduma za kiwango cha kimataifa ili kuongeza muda wa watalii kukaa nchini.

Konig amesema hoteli hiyo itakuwa ni sehemu ya mtandao wa hoteli zaidi ya 400 za Gran Melia.