Hotuba ya Lema haijasomwa bungeni

Wednesday April 24 2019
pic lema

Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuhusu maoni ya kambi ya upinzani bungeni ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 yanayotakiwa kusomwa bungeni jijini Dodoma leo. Kulia ni Msigwa akipinga kusoma maoni yaliyokuwa yakitambuliwa na Chenge huku akionyesha maoni aliyotaka kuyawasilisha bungeni hali iliyosababisha akasusa kusoma maoni hayo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekataa kusoma maoni ya upinzani katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwa madai kuwa Serikali imehariri na kuondoa mambo ya msingi.

Akizungumza leo Jumatano April 24, 2019 kwa niaba ya msemaji wa upinzani katika wizara hiyo, Godbles Lema, Mchungaji Peter Msigwa amesema nafsi yake na wenzake wa upinzani itamsuta kama atasoma maoni hayo aliyoyaita ni ya Serikali.

Mabishano ya Msigwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, yalianzia pale aliposimama na kuanza kusoma lakini kuna maneno ambayo aliyataja na Chenge akabaini kuwa hayakuwapo katika kitabu cha hotuba ya upinzani.

Maneno hayo yalizuiwa wakati msemaji huyo alipomaliza kusoma kuhusu adhabu aliyopewa mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema ambaye ni msemaji wa upinzani kwa wizara hiyo pamoja na madhila ya wapinzani kuhusu kesi akiwatia moyo kuwa ‘kesho ni bora kuliko jana’, lakini Chenge akamwelekeza msomaji kujielekeza katika kifungu kingine.

“Mheshimiwa Msigwa. Msigwa nakuomba usome maneno yaliyoko kwenye kitabu hiki ili twende kwa utaratibu mzuri tu, wala usitake tubishane,’’ amesema Chenge huku akiwa amesimama, kanuni zinamtaka Msigwa kukaa kitini.

Change alimtaka Msigwa kusoma yaliyoandikwa kwenye kitabu kilichoko mbele ya Bunge na kama hana cha kusoma basi aruhusu mjadala uendelee.

Advertisement

Alipopewa nafasi ya kuendelea na hotuba yake, Msigwa amesema hawezi kuendelea kusoma maneno ambayo yamehaririwa wakati wao ni wapinzani wanaotakiwa kuikosoa Serikali lakini wanaelekezwa cha kufanya.

 

“Nafsi yangu inanisuta na kwa niaba ya kambi ya upinzani sitaweza kusoma yale mnayotaka nisome sitakuwa nimetenda haki, hayo mnayotaka nisome mpeni Kangi (Lugola Waziri wa Mambo ya ndani) yeye atasoma,” amesema Msigwa.

Kabla ya kuanza kusomwa kwa hotuba hiyo, Mbunge wa Tarime Vijijini, Ester Matiko, amesimama kuomba mwongozo akihoji ni kwa nini hotuba za upinzani zinahaririwa na kuondoa maneno ambayo yalipaswa kujibiwa na Serikali.

Matiko ametumia kanuni ya 99, 64 na kanuni ya 15 zilizozungumzia kuhusu mambo ya upinzani bungeni.

Hata hivyo, Chenge ameeleza kuwa kilichoandika ndicho kitakachosomwa na akatumia kanuni ya 72 kuwa kauli ya Spika itakuwa ni ya mwisho katika kutoa uamuzi

Advertisement