VIDEO: Huu ndiyo mti wa mkuyu uliotumika kunyongea watu katikati ya jiji la Mwanza

Wakazi wa jiji la Mwanza wakipita jirani na sanamu la mti wa Mkuyu eneo la Kemondo,juzi, ambapo limejengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya kabila ya wasukuma waliutumia kutambika, kabla ya Uhuru wakoloni waliutumia kunyonga watumwa waliohukumiwa kifo. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Ni mti uliotumiwa na wakoloni wa Kijerumani kunyongea watu katikati ya jiji la Mwanza

Mwanza. Kiuchumi, Jiji la Mwanza ni kitovu cha biashara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutokana na uwezekano wa kufikika kirahisi kutoka miji mikuu ya mataifa wanachama.

Kwenye sekta ya utalii, jiji hilo pia ni kituo muhimu kutokana na urahisi wa kufikia mbuga na hifadhi za Taifa za Serengeti, Rubondo na Saanane ambayo ndiyo hifadhi pekee nchini inayopatikana katikati ya mji.

Likija suala la historia, jiji hilo pia haliko nyuma kwani ni kati ya maeneo yenye vivutio na kumbukumbu kadhaa tangu enzi ya ukoloni na baada ya uhuru.

Kwa mgeni anayefika jijini Mwanza kwa mara ya kwanza ataushangaa shina kubwa la mti lililopo kwenye mzunguko barabara ya Nyerere, Kenyatta na Makongoro karibu na ofisi za CCM mkoani Mwanza.

Mti huo aina ya mkuyu uliota wenyewe unaonekana vizuri ukitokea jengo la Benki Kuu (BoT) tawi la Mwanza lililo barabara ya Nyerere.

Kabla ya kuja kwa ukoloni, mti huo kwa mujibu wa wakongwe wa jiji ulitumika kwa shughuli za matambiko ya wenyeji.

Baada ya kuja kwa ukoloni, shughuli ya mti huo ilibadilika kutoka eneo la matambiko hadi kuwa sehemu ya kunyongea wakosaji waliotiwa hatiani wakati wa utawala wa Wajerumani.

Joseph Madereke (78) mkazi wa mtaa wa Msumbiji jijini Mwanza anasema baba yake, Christopher Madereka ni kati ya watu kadhaa waliohukumiwa adhabu ya kifo na Serikali ya kikoloni na kunyongwa kwenye mti huo mwaka 1899.

“Baba yangu alihukumiwa kifo kwa kunyongwa kutokana na kutiwa hatiani kwa kosa la kuunda kikundi maalum cha kuwapinga wakoloni,” anasema Madereke

Wakoloni kutoka Ujerumani walitawala Tanganyika (Tanzania Bara) kuanzia 1890 hadi 1918.

“Kwa mujibu wa maelezo ya wazee waliokuwepo wakati huo jiji la Mwanza halikuwa mji mkubwa kama lilivyo sasa; wanasema lilikuwa kama kijiji tu,” anasema Madereke

Anasema adhabu ya kifo ilitekelezwa kwa mkosaji kufungwa kamba shingoni na kuning’inizwa juu ya moja ya matawi ya mti huo hadi kufa.

Mzee Madereke anasema wengi wa walionyongwa walikuwa wale walioonekana kupinga baadhi ya matendo ya kikoloni ikiwemo kupora mashamba kwenye maeneo yenye rutuba na kuwatumikisha Waafrika.

Maelezo haya yanathibitishwa na Raphael Muruga (67) anayesema kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wazee, mjomba wake, Benedicto Merengo ndiye alikuwa mlinzi wa mti huo wa kunyongea Waafrika ‘wakorofi’ wasiokuwa watiifu kwa Serikali ya kikoloni.

Pamoja na ulinzi wa mti, Muruga anasema marehemu mjomba wake pia alikuwa akiwafundisha Wajerumani aina na maandalizi ya vyakula vya wenyeji.

Jiji la ukarabati

Baada ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961 mti huo uliendelea kusalia eneo hilo kama kumbukumbu ambayo hata hivyo hakujulikana kwa wengi.

Ofisa Uhusiano wa jiji la Mwanza, Elirehema Kaaya anasema ujenzi wa barabara ya Nyerere na mzunguko maarufu wa Mwanza-zero unaounganisha barabara ya Nyerere, Kenyatta na Makongoro, mti huo ulinyauka.

Anasema halmashauri ilifikia uamuzi wa kukata matawi yake na baadaye kulazimika kuukata na kusalia shina kutokana na ukubwa wake.

Anasema baadaye uongozi wa jiji uliamua kujenga sanamu maalum ya mti unaofanana na ule wa awali ili kudumisha historia ya eneo hilo.

Anasema pamoja na mambo mengine, ujenzi wa kumbukumbu hiyo imesukumwa na urafiki wa kindugu kati ya halmashauri ya jiji la Mwanza na jiji la Wurzburg nchini Ujerumani ulioanza tangu mwaka 1966 huku viongozi wa majiji hayo wakiwemo Mameya, Madiwani na Watendaji wakitembeleana.

Mwaka 2016 majiji hayo mawili yaliadhimisha miaka 50 ya urafiki na ushirikiano uliohusisha viongozi wa majiji hayo mawili kutembeleana.

Ziara hizo anasema ndiyo ilizaa wazo la kujenga sanamu ya kumbukumbu ya mti wa kunyongea kwa ajili ya historia ya mataifa ya Tanzania na Ujerumani.

“Siku zote huwezi kuifuta historia, iwe mbaya au nzuri daima itabaki kuwa tu historia; ndiyo maana licha ya historia ya mti ule kuwa na kumbukumbu inayoumiza miongoni mwa Watanzania, bado jiji limeona ni busara kuudumisha kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” anasema Kaaya

Ujenzi wa sanamu hiyo ulioanza Desemba 10, 2018 umekamilika Januari 28, 2019 ukigharimu zaidi ya Sh13.6 milioni zilizotolewa jiji dada la Wurzburg.

“Sanamu hii itakuwa moja ya vivutio vya utalii jijini Mwanza na halmashauri itafunga taa maalum ya umeme jua kuwezesha wageni kuuona mti huo kwa saa 24,” anasema Kaaya

Baada ya ujenzi kukamilika, Kaaya anasema mti huo utazinduliwa kwa sherehe maalum utakaoshirikisha makundi mbalimbali ya watu wakiwemo viongozi wa kiserikali, kijamii na wananchi wa kawaida.