Huyu ndiye Joyce Msuya bosi wa UNEP

Sunday March 24 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kuna orodha ndefu ya Watanzania walioaminiwa na mashirika ya kimataifa kushika nafasi kubwa, lakini wanawake wanaoingia kwenye orodha hiyo ni wachache.

Unaweza kumtaja Asha-Rose Migiro, ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Anna Tibaijuka, aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi la UN, au Dk Mwele Malecela ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hao ni kati ya wanawake wachache walio katika orodha fupi ya wanawake wa Kitanzania waliopigana hadi kufika kushika nafasi kubwa katika taasisi hizo.

Kati ya wanawake hao wachache yupo Joyce Msuya, ambaye mwaka jana aliteuliwa kuwa naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (Unep), ikiwa ni mafanikio makubwa ya safari yake iliyoanzia Shule ya Msingi ya Forodhani jijini Dar es Salaam.

“Sikuota kufika hapa, lakini nilifanya kazi kwa bidii sehemu nyingi kujiandaa kwa majukumu ya juu,” alisema Joyce wakati alipokutana na mwandishi wa gazeti la Mwananchi jijini Nairobi takriban siku kumi ziliopita.

Joyce na wenzake walikuwa Nairobi kuhudhuria mkutano wa mazingira wa UN uliofanyika kuanzia Machi 11 hadi Machi 15 kujadili masuala mazingira na athari zake.

Advertisement

Haikuwa rahisi kuwa na muda mrefu kuzungumza naye kutokana na majukumu mengi aliyokuwa nayo wakati huo pamoja na kuhitajiwa sehemu kadhaa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali.

“Nakupa dakika 15 tu uulize maswali yako kwa kuwa nimebanwa,” alisema Joyce nje ya jengo la mkutano huo mkuu wa UN Environment jijini Nairobi.

“Muda hautoshi kuongea kila kitu, naomba uulize maswali unayoona ni ya msingi tu.”

Lakini baadaye alikubali kufanya mahojiano kwa njia ya mtandao.

Joyce alikuwa kati ya zaidi ya watu 100 walioona tangazo la kumsaka naibu mkurugenzi mtendaji wa Unep na wakaomba na baadaye kuchujwa hadi kubakia tisa kutoka mataifa tofauti.

“Nilisailiwa kwa video conference (kufanyiwa usaili kwa njia ya video),” anasema.

“Mimi nilikuwa Washington DC na jopo la wakubwa watano wa UN lilikuwa Nairobi. Siku nne baada ya usaili nilipokea simu kunijulisha kuwa kati ya watu tisa waliosailiwa, nilikuwa namba moja na katibu mkuu, Antonio Gutteres anapanga kuniteua.”

Baada ya hapo, anasema walimuomba picha na akaambiwa asubiri mpaka katibu mkuu atakapotangaza kwenye vyombo vya habari, lakini majibu hayo yalishampa mwanga kuwa maombi yake yamefanikiwa.

“Nilifurahi sana kwa taarifa hizi. Nilitakiwa kufanya siri ila mtu wa kwanza kumwambia alikuwa mume wangu. Ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa Tanzania na wanawake duniani kote,” anasema Joyce katika mawasiliano kwa njia ya WhatsApp.

Taarifa ya uteuzi wake iliyotolewa Mei 21, 2018 na kuwekwa kwenye tovuti ya Unep, iligusia jinsi shirika hilo litakavyonufaika na uzoefu wake.

“(Joyce) ataleta kwenye taasisi hii uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 20 katika nyanja ya maendeleo ya kimataifa kutoka katika mashirika, uongozi na ushirika, akiwa amefanya kazi tofauti barani Afrika, Amerika Kusini na Asia,” inasema taarifa ya Unep.

Licha ya kutokea kwenye familia ya waziri mkuu wa zamani, Cleopa Msuya ambaye angemuwezesha kupata nafasi za juu kirahisi, Joyce anaamini katika kufanya kazi kwa bidii ili kufanikiwa.

“Daima naamini kufanya kazi ngumu na tofauti ili nijifunze na kukua kitaaluma. Ni kwa sababu hii nilishindana na kufanikiwa kuchaguliwa kwenye kazi za China, Korea Kusini na hapa Unep,” anasema Joyce.

“Tuzoee kufanya kazi na vitu vigumu ambavyo vinaweza kututofautisha na wengine. Pale tutakaposhindwa, tujiulize kwa nini hatukufanikiwa ili tujifunze na kusonga mbele.”

Tangu akisoma shule ya msingi, Joyce anasema alikuwa anapenda kufanya kazi ngumu, tena kwa bidii akikusudia kuifanikisha kwa zaidi ya asilimia 100. Moyo huo umemuwezesha kupata nafasi ya kufanya kazi nchi mbalimbali akiwa na Benki ya Dunia.

Licha ya kuwa mama wa watoto wawili, Melanie na Ethan, bosi huyo wa Unep anasema kufika kwake nafasi hiyo ya sasa kunatokana na juhudi na uthubutu wa kujaribu mambo magumu ili kukua kitaaluma.

Nafasi hizo zimemuwezesha Joyce kusafiri sehemu mbalimbali duniani.

“Sikusahau nilikotoka wala thamani yangu kama binadamau na umuhimu wa familia na marafiki,” anasema.

“Yote haya yamenisaidia kunipa upeo mpana wa maisha, binadamu na mataifa tofauti.”

Pamoja na kuamini katika bidii na kufanya mambo magumu na tofauti, Joyce anaona mume wake, watoto na familia yao wana mchango mkubwa katika mafanikio yake.

Anasema kuanzia wazazi hadi watoto wake, kila mmoja kwa nafasi yake amechangia kwa kiasi chake.

“Wazazi walinifundisha kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu watu wote na kutosahau nilipotoka, hii ni kuanzia nyumbani kwetu Usangi,” anasema.

“Kama usingekuwa mwongozo wenye upendo wa marehemu mama yangu, Rhoda na baba (Cleopa Msuya), huenda nisingefika nilipo.”

Anasema tangu anakua, wazazi wake walimsisitiza kufanya kazi kwa bidii na kumshauri asome masomo ya sayansi, kwenda kanisani na kumheshimu Mungu pamoja na kuonyesha upendo kwa watu wote bila kujali daraja au tabaka.

Anasema ilikuwa kawaida kila likizo kupelekwa Usangi ili kufahamiana na ndugu na kupata nafasi ya kujitolea kwa jumuiya.

“Wanangu wananipa malengo ya maisha. Wananikumbusha umuhimu wa kuwa na vipaumbele. Familia yangu yaani kaka, dada, mawifi na mashemeji zangu ni mtandao wangu wa mshikamano na upendo,” anasema.

Kuhusu mume wake, Joyce anasema ni baraka nyingine kwenye maisha yake kwa kuwa amekuwa akimpa kila aina ya ushirikiano anaouhitaji kwa wakati. Hali hiyo anasema imedumu kabla hata baada ya kupata watoto wao wawili.

“Tulikutana na kufahamiana Dar es Salaam na tulioana Septemba 12, 1998. Nimeweza kufika nilipo kwa kuwa tupo timu moja katika safari yetu,” anasema.

Kupambana na mataifa mengine 

Pamoja na kufanikiwa kuongoza taasisi hizo akiwa na nafasi tofauti, Joyce anasema kupata mafanikio kunahitaji kuwa tayari kupambana na watu kutoka mataifa mengine.

“Ni shughuli inayohitaji uvumilivu na kujituma zaidi,” anasema.

“Zipo nafasi lakini zote ni za kushindaniwa hivyo kwa Mtanzania yeyote anayependa kutoka ni lazima ajiandae kupambana na wafanyakazi wa nchi nyingine.”

Lakini anasema pamoja na sifa nyingine za jumla, elimu ya kutosha inahitaji na hivyo ni vizuri kufanya jitihada kujiendeleza.

Pia anasema Serikali inaweza kusaidia kuwapenyeza Watanzania kwenye taasisi na mashirika ya kimataifa kwa kupendekeza majina ya wenye sifa na vigezo vya kushindania kazi Umoja wa Mataifa kwa kuwa ajira zilizopo katika taasisi hizo hutangazwa na ni lazima zigombewe.

Pia anaona iko fursa kwa wanawake wengine kufika ngazi aliyopo au zaidi ya hapo ila, anashauri haja ya kufanya kazi kwa bidii na kupata elimu ya juu kadri inavyowezakana. Anasema ni lazima wajifunze shughuli ngumu kwa kuwa wanawake wanatakiwa kupambana zaidi na maisha pamoja na majukumu ya kazini bila kusahau kulea.

“Tanzania tumebarikiwa sana. Nimeishi na kufanya kazi mabara yote duniani, nchi yetu imebarikiwa rasilimali nyingi sana na idadi kubwa ya watu, tuna uwezo wa kuleta maendeleo kwa wananchi wote.”

Anasema changamoto zipo kila mahali lakini anasisitiza kutokata tamaa na kuwa na upeo mpana wa maisha binafsi na maendeleo kwa vizazi vyetu na vijavyo.

Safari ya Joyce UN
Joyce Msuya, ambaye ni mama wa watoto wawili alizaliwa Januari 2, 1968 jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Ocean Road. Alisoma elimu ya msingi Shule ya Forodhani na baadaye kwenda Shule ya Sekondari ya Jangwani, ambako alisoma kwa miezi sita kabla ya kuhamishiwa Weruweru ambako alisoma hadi kidato cha sita.
Baadaye alikwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Strathcyde nchini Scotland.Ni mhitimu wa sayansi ya viumbehai wadogo na ana shahada ya umahiri (microbiology and immunology) kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa nchini Canada.
Elimu hiyo imemfanya ashike nafasi za juu katika mashirika makubwa duniani.
Kabla ya uteuzi huo, Joyce alikuwa mwakilishi maalumu wa Benki ya Dunia na mkuu wa ofisi ya Jamhuri ya Korea, hali kadhalika mratibu wa kanda wa Taasisi ya Benki ya Dunia iliyokuwa na ofisi zake nchini China, lakini ikihusika na nchi za Asia Mashariki na Kanda ya Pasific, na pia ofisa mkuu wa mikakati wa Idara ya Huduma, Viwanda na Biashara ya Shirika la Kimataifa la Fedha.

Advertisement