Idi Amin avunja daraja la Mto Kagera - 4

Muktasari:

Jana tuliona jinsi majeshi ya Idi Amin wa Uganda yalivyoshambulia ardhi ya Tanzania na jinsi kiongozi huyo wa Uganda alivyokuwa akiiambia dunia kuhusu mashambulizi hayo. Kitendo hicho kilimuudhi Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamua kuitisha mkutano wa viongozi mkoani Dar es Salaam na kutoa ile hotuba maarufu ya “sababu za kumpiga tunazo, nia ya kumpiga tunayo na uwezo wa kumpiga tunao”. Mwalimu Nyerere alielezea kwa kina jinsi Tanzania ilivyopuuzia madai ya Idi Amin hadi alipofanya uamuzi huo wa kujibu mashambulizi. Sasa endelea...

Baada ya amri ya Rais Julius Nyerere aliyoitoa Jumatatu ya Oktoba 30, 1978 ya kutaka Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuingia vitani, Brigedi ya Kusini ilipewa jukumu la kuanza kujibu mashambulizi.

Brigedi ya Kanda ya Kusini iliyokuwa na makao yake huko Songea, chini ya Brigedia James Luhanga, ilikuwa na wapiganaji kati ya 4,000 na 5,000. Kwa mujibu wa gazeti The Citizen la Oktoba 14, 2014, halikuwa jambo la bahati mbaya kwamba brigedi hiyo kuwa tayari kwa vita.

“Brigade hii ilikuwa imeandaliwa ili baadaye iweze kutumwa nchini Namibia kujiunga na askari wa msituni wa Swapo,” linaandika gazeti hilo.

Brigedi hiyo ilianza safari Alhamisi ya Novemba 2, 1978, siku ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa akilitangazia taifa kuhusu “uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania kumpiga”.

Askari wa brigedi hiyo walilazimika kusafiri na zana zao za kivita kwa umbali wa kilometa 1,600 kutoka Songea hadi uwanja wa vita.

Baada ya safari hiyo ya tabu kubwa kutokana na mvua iliyokuwa inanyesha na barabara kuharibika vibaya, wanajeshi waliwasili na mara moja kuanza kuchimba mahandaki kwa ajili ya kujihifadhi kwa shambulizi lolote la anga ambao halikutarajiwa.

Mjini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine alitoa maelekezo kwa wakuu wote wa mikoa 20 ya Tanzania kuhamasisha matumizi ya mali za serikali na za watu binafsi kutumika katika vita.

Mabasi na malori kutoka serikalini na kwa kampuni binafsi yalitumika kupeleka wapiganaji na vifaa kwenye viwanja vya vita. Kwa watu waliokuwa na magari mabovu waliiona fursa hiyo kwa sababu magari yao yalifanyiwa matengenezo.

Ingawa yaliteka eneo la Kagera kwa urahisi, majeshi ya Idi Amin yalihofia sana Jeshi la Tanzania kujibu mapigo. Waandishi wa kitabu cha Deadly Developments, Stephen na Downs Reyna wameandika katika ukurasa wa 117 kuwa kwa kuhofia hilo, wanajeshi wa Uganda waliamua kulipua daraja la Mto Kagera eneo la Kyaka.

Toleo la 348 la jarida New African liliandika kuwa “huu ulikuwa mwanzo wa mwisho wa utawala wake (Idi Amin)” nchini Uganda.

Luteni Kanali Marajani wa Uganda alitumia ndege za MiG kulipua daraja hilo. Kazi hiyo ilifanyika Novemba 1 na 2, lakini walishindwa kuliharibu daraja hilo la Kagera. Wanajeshi wa Tanzania walizirushia makombora na baadhi ya ndege hizo zilitunguliwa. Marubani waliobakia wakavunjika moyo wa kuendelea na kazi hiyo.

Baadaye Marajani akapata wazo la kutumia bomu la kutegwa. Akaenda machimbo ya shaba ya Kilembe, kiasi cha kilometa 225 kwenye milima ya Ruwenzori. Meneja wa machimbo hayo, ambaye alikuwa Mwingereza, alikubali na akatuma timu yake ya wataalamu kwenda kutega mabomu daraja la Mto Kagera.

Usiku wa Ijumaa ya Novemba 3, 1978, wategaji wa mabomu hayo walifika darajani na kufanya kazi hiyo bila kuonekana. Kabla ya kupambazuka daraja likawa limelipuliwa. Mmoja wa wanajeshi wa Uganda aliyekuwa na watega mabomu hayo ni Sajini Kifulugunyu.

Kifulugunyu aliliambia gazeti Daily Monitor la Uganda (Aprili 23, 2016) kwamba wataalamu hao wa mabomu walikuwa watatu, lakini utafiti wa gazeti hilo uligundua kuwa walikuwa wanne—Muitaliano mmoja na Waganda wanne.

Baada ya hapo, ilikuwa ni furaha tele.

“Tulifanya sherehe hapa hadi Kampala. Tuliridhika kuwa Jeshi la Tanzania halingeweza kutushambulia tena baada ya kuharibu daraja ambalo wangetumia kuvuka na kuingia Uganda,” Kifulugunyu aliliambia gazeti hilo.

Mmoja wa marubani waliotumika kujaribu kulilipua daraja hilo ni Meja John Amunga (maarufu kwa jina la Kassim Semugabi). Alikuwa mmoja wa marubani bora zaidi wa kijeshi wa Jeshi la Uganda, akiendesha ndege aina ya MiG-21. Wanajeshi wenzake walimbatiza jina la “Mharibifu wa Tanzania”.

Mwingine alikuwa ni John Carse kutoka Seychelles na ambaye alikuwa ni mtaalamu wa ubomoaji. Ndiye anayedaiwa kuwa alilipua daraja hilo.

Lakini, katika ukurasa wa 149-150 wa kitabu cha Guardian Angel: The Moshi Conspiracy kilichoandikwa na Arnold Spero Bisase, kuna maelezo tofauti.

Aliyekuwa mfungwa wa Tanzania ambaye hakutaka jina lake litajwe, na ambaye wakati kitabu hicho kinaandikwa mwaka 2012 alikuwa anaishi nchi za Scandinavia, alimwambia mwandishi wa kitabu hicho kuwa aliwahi kuwa katika gereza moja na John Carse mkoani Dodoma ambako aligundua kuwa raia huyo wa Seychelles hakuhusika kulipua daraja hilo.

Siku daraja hilo lilipolipuliwa, JWTZ ilikumbana na kikwazo kingine. Ndege zake tatu zilikuwa zikitoka uwanja wa ndege wa Ngerengere mkoani Morogoro kuelekea Mwanza, zikapita juu ya Ziwa Victoria ambako askari wa JWTZ walishaambiwa wakae chonjo.

Kitengo cha Musoma hakikuwa na taarifa ya kuwasili kwa ndege hizo. Ndege zote tatu zililipuliwa kwa makombora na kuua marubani wake.

Akilitangazia Taifa tukio hilo, kwa masikitiko Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Katika mambo ya vita ajali hutokea, na vijana hawa walikwishaambiwa ndege zikionekana zipigwe. Wangeziacha? Wanajuaje ni za adui? Kwa hiyo ikatokea bahati mbaya hiyo.

“Matukio haya hatukuyatangaza. Hata kule kupigwa kwa ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno. Tulisema akiendeleaendelea kuleta ndege zake, tutaendelea kuziangusha kila zinapokuja.”

Mara baada ya maneno hayo, alipanda ndege kwenda Beira, Msumbiji kukutana na Rais Samora Machel na kushauriana juu ya uvamizi wa Idi Amin. Nyerere alimwambia Machel kuwa kikosi cha Jeshi la Tanzania kilichokuwa kwenye mpaka wa Msumbiji na Rhodesia (Zimbabwe) kilirudi Tanzania kwa ajili ya Vita ya Kagera.

 

 

 

Itaendelea kesho