VITA YA KAGERA: Luteni alivyoziingiza vitani Tanzania na Uganda-1

Muktasari:

  • Kuanzia leo tutawaletea makala mfululizo kuhusu Vita ya Kagera kati ya Tanzania na Uganda iliyodumu kwa miezi sita. Vita hiyo ilianzia Kagera kabla ya kuhamia Uganda ambako majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na ya Uganda yalimuondoa kiongozi wa kijeshi wa wakati huo nchini Uganda, Idd Amin Dada. Fuatilia safu hii upate ufahamu au kumbukumbu ya vita hiyo ya kihistoria kuwahi kutokea Tanzania.

Vita kati ya Tanzania na Uganda, au Vita ya Kagera ilidumu kwa miezi sita kuanzia Novemba 1978 hadi Aprili 1979. Vita hiyo ndiyo iliyouangusha utawala wa Idi Amin Dada uliodumu kwa muda wa miaka minane.

Idd Amin aliingia madarakani Jumatatu ya Januari 25, 1971 alipoiangusha serikali ya Dk Milton Obote na aliondoka Jumatano ya Aprili 11, 1979 wakati majeshi ya Tanzania na ya Uganda yaliposhirikiana kumuondoa.

Mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda ulianza Jumatatu ya Januari 25, 1971 baada ya Amin kuipindua Serikali ya Dk Obote. Muda mfupi baada ya hapo, Rais wa Tanzania alimpa Dk Obote hifadhi ya kisiasa. Akiwa Tanzania Dk Obote alianza mipango ya kurejea Uganda akitumia ardhi ya Tanzania.

Mambo mengi ambayo yangeweza kusababisha Vita ya Kagera yalikuwa yametendeka tangu Januari 1971 hadi Oktoba 1978, lakini kwa kipindi chote hicho hakuna vita iliyozuka.

Vita hiyo ilianza rasmi siku ileile ya maadhimisho ya Uhuru wa Uganda, yaani Jumatatu ya Oktoba 9, 1978 baada ya mwanajeshi mmoja wa Uganda kuvuka mpaka na kuingia Tanzania kupata kinywaji na kukutana na mpenzi wake ambaye alikuwa raia wa Tanzania.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda la Jumanne ya Oktoba 9, 2017, wakati mwanajeshi huyo akiwa mpakani upande wa Tanzania kwa starehe zake, alijikuta akipambana na wanausalama wa Tanzania.

Mwanajeshi huyo alikamatwa na kuwekwa rumande. Mapema asubuhi ya siku iliyofuata, aliachiwa aondoke. Kwa kudhani amedhalilishwa na wanausalama wa Tanzania, alikimbilia kambini kwake upande wa Uganda, akachukua bunduki na kurejea upande wa Tanzania kulipiza kisasi.

Alipofika umbali fulani kutoka kituo alichokuwa ameshikiliwa, alifyatua risasi kwa mbali. Askari wa zamu wa kituo hicho walilazimika kukimbia. Hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa.

Alipojisikia vizuri kwa kitendo hicho, aliamua kurejea kambini kwake upande wa Uganda na kumdanganya kamanda wa kikosi chake aliyejulikana kwa jina la Luteni Byansi kwamba alitekwa na askari wa Tanzania, lakini akapambana nao.

Bila kutafakari sana, Luteni Byansi alimpigia simu Kamanda wa Kikosi cha Malire (MMRR) kilichoko Lubiri mjini Kampala, Kanali Juma Ali Oka (alikuwa maarufu kama Juma Butabika).

Bila kuwajulisha maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Uganda (UPDF), Kanali Butabika aliviamuru vikosi vya jeshi vilivyokuwa Ziwa Victoria kwenda kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Luteni Byansi kuishambulia Tanzania.

“Nilikuwa kamanda wa kwanza wa vifaru kuingia Tanzania. Tuliamriwa kushambulia. Tulikaa Tanzania kwa wiki mbili kabla ya kuamriwa kuondoka na kurejea Uganda,” Luteni Muzamir Amule wa UPDF alimwambia mwandishi Faustine Mugabe wa Daily Monitor katika mahojiano aliyofanyiwa mwaka 2015 nchini Uganda.

Kwa maoni yake, Kanali Butabika aliingiza Uganda vita isiyo na ulazima wowote.

“Unawapelekaje vitani wanajeshi kutoka Malire (Kampala) hadi Mutukula (Tanzania) bila kumtaarifu Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama au hata kamanda yeyote wa juu wa jeshi?” anahoji Luteni Amule katika habari hiyo.

Ijumaa ya Oktoba 27, 1978, mara baada ya uamuzi wa Kanali Juma Butabika, zilitumwa ndege tatu za kivita aina ya ‘MiG-21’ (Mikoyan-Gurevich) za Kirusi. Marubani bora zaidi wa ndege hizo nchini Uganda, Luteni David Omita, Luteni Atiku na Luteni Abusala walichaguliwa kwa kazi hiyo maalumu.

Kumbukumbu nyingine zinaonyesha kulikuwa na rubani mwingine aliyeitwa Walugembe. Mwaka mmoja kabla, marubani hao watatu—Luteni Omita, Luteni Atiku na Luteni Abusala—walikuwa wamerejea kutoka mafunzoni nchini Urusi.

Uganda ilinunua ndege 20 za aina hiyo mwaka 1977 kuziba pengo la zile aina ya MiG-15 zilizoharibiwa Jumapili ya Julai 4, 1976, wakati makomandoo wa Israel walipoivamia Uganda katika shambulio linalojulikana kama Operation Entebbe.

Ndege hizo zilipaa kutoka Entebbe kwenda kuishambulia Tanzania. Ndani ya muda mfupi zikawa zimeshambulia na kurejea Uganda.

Zilipogeuka, ndege ya Luteni Omita ilipigwa kombora na wanajeshi wa Tanzania. Kombora hilo liliharibu bawa lake la kushoto na ikashika moto. Lakini kati ya sekundi chache kabla ya kushika moto, Luteni Omita alifanikiwa kuruka kwa parachuti.

Hadi wanajeshi wa Tanzania wanafika yalipokuwa mabaki ya ndege hiyo, rubani huyo alikuwa ameshatoweka.

Nchini Uganda, wanajeshi wenzake wakiamini kuwa Luteni Omita ameuawa na majeshi ya Tanzania, walimwona akirejea kambini kwa mguu. Baadaye alipelekwa Entebbe kukutana na Idi Amin ambaye alimpongeza kwa ujasiri wake.

Jumapili ya Oktoba 29, 1978, kwa mujibu wa matangazo ya kituo cha redio cha Voice of Uganda ya Oktoba 30, 1978, Idi Amin aliwapandisha vyeo Omita, Atiku, Abusala na Walugembe kuwa makanali na kuwafanyia tafrija.

Tafrija ya kuwapandisha vyeo ilifanyika mjini Entebbe kwenye Uwanja wa Ndege wa Jeshi.

Wakati Idi Amin akiwa katika sherehe hiyo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilifanya shambulio lake la kwanza kabisa eneo la Kikagati ndani ya Uganda na kuingia kilometa kadhaa bila ya upinzani wowote.

Itaendelea kesho