Jafo alaani matumizi ya nguvu kubwa kwa raia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) Selemani Jafo

Muktasari:

Waziri Jafo akiwa katika mazishi ya Isaka Petro aliyefariki baada ya kutokea vurugu kanisani, amelaani vitendo vya kutumia nguvu kubwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa umma.


Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) Selemani Jafo amelaani matumizi ya nguvu kubwa yanayofanywa na baadhi ya watumishi wa umma dhidi ya wananchi na kuleta machafuko yanayosababisha mauaji kwa raia wasio na hatia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya wizara hiyo, Jafo alitoa kauli jana Febuari 5, 2019 wakati wa mazishi ya marehemu Isaka Petro aliyefariki Jumamosi baada ya kutokea vurugu katika Kanisa la Waadventisti Wasabato Itigi kundi Namba Mbili .

Petro alizikwa jana nyumbani kwao Kijiji cha Kazikazi kata ya Kitaraka wilayani Manyoni mkoani Singida na mazishi yalihudhuriwa pia na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ikiongozwa na mwenyekiti wake Dk Rehema Nchimbi.

Jafo ambaye ni mbunge wa Kisarawe amesema “Tukio hili lilitokea si agizo la Serikali na waliotekeleza wamefanya kwa utashi na akili zao binafsi. Hawakuagizwa na mtu yeyote na zaidi wametenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma.

“Hakuna namna tunaweza kusema vinginevyo kuhusu tukio hili zaidi ya kuwa tukio baya na la kusikitisha sana kuwahi kutokea kwa wananchi wetu. Mbaya zaidi limetekelezwa na watumishi wa Serikali inasikitisha sana, nawasihi watumishi wa umma tutangulize utu mbele kwenye kila kazi tunazozifanya,” amesema Jafo katika mazishi hayo.

Jafo amewasisitizia watumishi wa umma kutanguliza ubinadamu mbele katika majukumu yao haijalishi unafanya kazi gani na katika mazingira gani.

Amewataka watumishi hao kuwaunganisha wananchi na kuwafanya kuwa kitu kimoja na si kuwa kichocheo cha ugomvi  na mafarakano dhidi yao.

“Kwa taarifa nilizopewa na nimezithibitisha ni kuwa wote waliohusika na tukio hili wameshakamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na taratibu zao,”anasema .

Dk Nchimbi amesema kuwa msiba huo ni pigo kwa Serikali na wananchi wote wa kijiji cha Kazikazi kwa kuwa Serikali inawahudumia wananchi walio hai na si wafu lakini inapotokea raia anaondoka duniani kwa kifo cha namna hiyo ni pigo kubwa.

“Serikali tuna wajibu wa kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wananchi wetu kufanya shughuli zao kwa usalama wa hali ya juu sasa wajibu huu unapotekelezwa kinyume na taratibu zetu ni makosa. Kila mtu atawajibika kwa kadri ya kosa lake,’’ amesema Dk Nchimbi.

Mchungaji wa Kanisa la Waadiventista Wasabato Itigi Kundi Namba Mbili, Manigina  Manigina amewaasa wanakijiji cha Kazikazi kutokuwa na kisasi na kumuomba Mungu ili tukio kama hilo lisitokee tena katika kijiji chao.

“Visasi ni vya Mungu, nyinyi msiweke visasi na mtu ila endeleeni na maisha yenu kama kawaida na Mungu atazidi kuwashushia baraka zake katika kazi zenu,”amesema.