Jicho la wasomi na ushirika huru wenye demokrasia

Wasomi na wanaharakati wa masuala ya kijamii wamekubaliana kwamba njia inayoweza kuihakikishia Tanzania maendeleo endelevu yenye manufaa kwa wananchi ni ushirika badala ya njia kuu za uzalishaji mali kumilikiwa na watu binafsi.

Hayo yamejitokeza katika mjadala uliofanyika mwishoni mwa wiki ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia idara yake ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma, kwa kushirikiana na Kavazi la Mwalimu Nyerere (NRC).

Mjadala huo uliohudhuriwa na wasomi, wanafunzi, wanaharakati na wataalamu wa masuala ya maendeleo, ulikuwa ni hitimisho la mafunzo ya wiki moja kuhusu ushirika yaliyoandaliwa na Kavazi na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.

Ukifanyika chini ya mada iliyopewa jina la “Kutoka mali za mtu mmoja kwenda kwenye mali za watu wengi,” watoa mada pamoja na wachangiaji walibainisha kwamba ili juhudi za kutokomeza umasikini ziweze kuzaa matunda, serikali haina budi kuupa kipaumbele ushirika ili kupunguza pengo la kipato baina ya wananchi.

Muungano wa hiari

Wataalamu wanaulezea ushirika kama muungano wa hiari wa watu waliokubali kuendesha shughuli zao za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa pamoja ili kuinua hali zao za maisha.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), mpaka kufikia Desemba 2017, Tanzania ilikuwa na jumla ya vikundi vya ushirika vipatavyo 10,990 vikiwa na wanachama wapatao 2,619,311.

Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na jumla ya vikundi vya ushirika 1,094 vyenye wanachama 327,811. Vyama vya akiba na mikopo (Saccos) vinaongoza kwa kuchukua asilimia 54 ya vikundi vyote vya ushirika nchini vikifuatiwa na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ambavyo vinachukua asilimia 31.

Mjadala huo ulifanyika katikati ya mjadala mpana wa kitaifa kuhusu dhamira ya serikali ya kutaka kujenga uchumi wa viwanda na kujenga Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Swali linalosumbua sasa ni endapo Serikali iendelee kumtegemea mkulima mdogo ili kufanikisha nia yake au iendelee kutegemea wakulima wenye mitaji mikubwa kwa uzalishaji kama vile kilimo cha kisasa.

Mmoja kati ya wasomi waliohudhuria mjadala huo ni Profesa Issa Shivji ambaye aliwaeleza washiriki kwamba mjadala huo ni umuhimu katika kipindi hiki ambapo Serikali inasema imedhamiria kufanya mageuzi katika uendeshaji wa nchi.

“Hii ni kwa sababu tukiongelea uzalishaji wa kilimo ni wazi kwamba tunaongelea uzalishaji wa mkulima mdogo, ambaye kwa wastani hamiliki zaidi ya ekari mbili za ardhi,” alisema Shivji.

Shivji ambaye pia ni mwenyekiti wa NRC, anasema licha ya ukweli kwamba mkulima mdogo amekuwa msingi wa uzalishaji wa ziada yote kwa Taifa, bado amekuwa sehemu ya jamii inayonyonywa zaidi tangu hapo zamani na hadi sasa.

Na kwa sababu kihistoria inaonyesha kwamba mkulima mdogo anakuwa ni mwanamke, hivyo unyonyaji huu umekuwa ukimgusa yeye kwa kiwango kikubwa.

Ushirika kunyanyapaliwa

Lakini, Shivji ana angalizo zaidi “nchi hii ushirika unanyanyapaliwa sana kutokana na yale yaliyotokea katika historia...Lakini, mimi bado napendekeza ushirika kama njia sahihi ya uendeshaji wa masuala ya nchi. Ni muhimu tukawa na ushirika katika kila sekta, iwe ni kilimo, ulaji, usafirishaji, nk.”

Historia anayoizungumzia Profesa Shivji ni ile ya uingiliaji kidola kwa vyama vya ushirika, kitu ambacho kilisababisha kufa kwa vyama vingi.

Vyama vingi vilianzishwa kwa muundo wa juu-chini, yaani kwa msaada wa dola na wala haikuwa mipango ya kutoka wananchi wenyewe.

Ilipofika mwaka 1966, vyama vingi vya ushirika vilikuwa vimejaa urasimu na ufisadi na wakulima wengi wakawa wanavilalamikia, kwamba vimeondosha madalali binafsi na kuweka madalali wa kivyama.

Urasimu huu ulishika hatamu baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967, ambapo urasimu wa kidola ulikabiliana na urasimu wa vyama vya ushirika na hatimaye ushirika ukapigwa marufuku miaka ya 1975-6, kosa ambalo Mwalimu Julius Nyerere alikuja kujutia baadaye.

Vyama vya ushirika vilirudi tena mwaka 1992 lakini wakati huo nchi ikiwa iko katikati ya shida za kubwa kiuchumi.

Dhana ya ushirika na demokrasia

“Ushirika huwawezesha wananchi kufanya kitu ambacho mmojammoja hawawezi kufanya,” anabainisha Professa Shivji, akisisitiza uwepo wa uhuru wa uendeshaji wa chama husika bila ya kuingiliwa na dola kama msingi wa mafanikio wa ushirika.

Anaongeza kuwa “hii huongeza uwezo wa kupatana wa wazalishaji wadogo katika soko dhidi ya wafanyabiashara wakubwa.”

Kitu cha msingi katika ushirika ni utayari wa washirika wenyewe kushirikiana kwa hiari yao kuboresha hali zao za maisha, anafafanua Profesa Hamudi Majamba kutoka UDSM.

Profesa Majamba ambaye alikuwa moja kati ya waongeaji wakuu katika mjadala huo, alifafanua kuwa demokrasia ni kitu muhimu katika ushirika. Serikali haitakiwi kujishughulisha na shughuli za ushirika, itoe fursa kwa washirika kuendesha mambo yao kwa uhuru.”

Athari ya serikali kuingilia vyama vya ushirika, kwa mujibu wa Profesa Majamba, ni kama yale yaliyotokea kwenye zao la korosho ambapo yeye anadhani serikali iliingilia kazi ambayo kimsingi ilipaswa kufanywa na vyama vya ushirika.

“Serikali zimekuwa zikiwatumia wakulima wadogo na kuwatelekeza,” anabainisha Profesa Majamba.

Ushirika na maendeleo

Akizungumzia jinsi ushirika unavyoweza kuleta maendeleo ya nchi, Profesa Kannimel Hirilal kutoka Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, kilichopo nchini India anasema msingi wa maendeleo ya nchi kama Tanzania ni kilimo, kwani ndiyo kitaweza kutoa malighafi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.

“Sasa watu wenye mitaji mikubwa hawavutiwi na kilimo na hivyo hununua ardhi na kuiacha bila ya matumizi ili kuja kuiuza baadaye kwa bei ya juu itakayowaingizia faida. ,” anasema Profesa Hirilal.

Anaongeza kwamba kitu pekee kinachoweza kuokoa hali hii ni ushirika.

“Kwanza ushirika huwazuia wenye mitaji mikubwa kujilimbikizia ardhi kwa kuinunua kwa bei rahisi kutoka kwa mkulima mmojammoja. Pili ni kwamba ushirika, kwa kushirikiana na serikali ya mtaa husika, unaweza kuitumia ardhi yake kwa mahitaji ya jamii husika tofauti kama ingekaa tu kusubiri kuuzwa.”