Kampuni ya Kenya kununua korosho kwa Sh Sh418 bilioni

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na kampuni ya Indo Power Solutions Limited ya nchini Kenya kuiuzia korosho tani 100,000 kwa gharama ya Sh418 bilioni


Arusha. Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko  nchini Tanzania imeingia mkataba na kampuni ya Indo Power Solutions Limited ya nchini Kenya kununua tani  100,000 za korosho yenye thamani ya Sh418 bilioni  msimu wa mwaka 2018/19.

Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa akizungumza jana jioni Januari 30, 2019  amesema kiwango hicho kinawezesha wakulima kunufaika na jasho lao baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku kununua korosho kwa bei inayomkandamiza mkulima.

“Msimu huu inakadiriwa tutakusanya tani 240,000 na katika kiwango hicho tayari tumeshakusanya tani 213,159 pia tani 129,194 zimeshahakikiwa na wakulima wetu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani wameshalipwa fedha zao ambazo ni Sh416.4 bilioni kufikia Januari 28, 2019,” amesema Bashungwa.

Amesema kiwango cha korosho kilichohakikiwa na kiasi ambacho kimelipwa ni  asilimia 95.7 na kwamba Serikali inaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli kwamba ifikapo Februari 5, 2019 wakulima wote wawe wamelipwa.

Mkurugenzi  Mtendaji  wa kampuni hiyo, Brian Mutembei  ameishukuru Serikali ya Tanzania kukubali kampuni yake kununua korosho hiyo kati ya makampuni 18 yaliyoonesha nia ya kufanya biashara na Tanzania.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema utaratibu wa kisheria wa kuingia mikataba umefuatwa kikamilifu chini ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, umefika wakati wa kuanza kuuza Korosho hizo kwenye soko la kimataifa.

“Tumekubaliana mara baada ya kuweka saini mkataba huu ndani  ya wiki moja malipo yote yatakua yamefanyika  na mnunuzi ataanza kuibeba Korosho yake baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuisomba na kuikusanya kwenye maghala,” amesema Kabudi.