Kampuni ya korosho yatikisa Bunge

Sunday May 19 2019
pic korosdho

Mbunge wa Tarime vijijini (chadema), John Heche akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Dodoma juzi. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Kampuni ya Kenya ya Indo Power iliyojitokeza kununua korosho nchini na kushindwa kufanikisha mpango huo imesababisha mvutano mkali bungeni baada ya wabunge wa upinzani kushinikiza mawaziri walioileta nchini kuwajibishwa huku Serikali ikiwakingia kifua ikidai hawahusiki.

Januari 30, Serikali kupitia Bodi ya Nafaka ya Mazao Mchanganyiko (CPB) iliingia makubaliano na kampuni hiyo ya kununua korosho tani 100,000 ambayo yangeipa Serikali dola za Marekani 180.2 milioni (Sh418 bilioni).

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda wakati akihitimisha bajeti ya wizara yake Jumatano iliyopita alisema Serikali imevunja mkataba huo kutokana na kampuni hiyo kushindwa kutimiza matakwa ya makubaliano.

Maelezo hayo ya Waziri Kakunda yaliibua mvutano mkali bungeni kwa upinzani kumtaka aliyekuwa waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga waliokuwepo kushuhudia makubaliano hayo wawajibishwe na kujiuzulu nafasi zao.

Katika mjadala wa juzi wa bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2019/20 ya Sh253.85 bilioni, hotuba ya upinzani ya wizara hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga alisema licha ya mkataba huo kupigiwa debe na Profesa Kabudi (sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje) na Gavana Profesa Luoga kambi hiyo inaitaka Serikali kuwawajibisha wawili hao.

Haonga alisema, “wahusika hawa wamelipotosha taifa na kuliingiza hasara kubwa kutokana na mkataba ambao haukufanyiwa upembuzi yakinifu.”

Advertisement

Mchuano mkali ulijitokeza juzi jioni wakati wabunge wa upinzani wakichangia bajeti hiyo. John Heche (Tarime Vijijini-Chadema), Hamidu Bobali (Mchinga-CUF), Cecil Mwambe (Ndanda-Chadema) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema) walichuana vikali na mawaziri; Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya.

Wakati wabunge hao wakitaka Profesa Kabudi awajibishwe, kaimu kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ambaye ni waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisimama na kumtetea Profesa Kabudi kuwa uamuzi ule haukuwa wake peke yake bali ulikuwa ni uamuzi wa mawaziri wote.

Mchungaji Msigwa alisema Profesa Kabudi ni msomi na ndiye aliyeishauri kampuni ya Indo Power ya Kenya inunue korosho wakati haikuwa na uwezo, hivyo anapaswa kuwajibishwa.

“Tunampongeza Rais kwa kuchagua wasomi, lakini tuliamini Profesa angeweza kuwa na uelewa mpana wa kumshauri Rais na Taifa lakini ametuingiza chaka, lazima aachie ngazi,” alisema Msigwa.

Hata hivyo, Waziri Mwakyembe aliposimama kutoa taarifa alisema mawaziri wanawajibika pamoja, hivyo jambo lolote linalotendeka ni kwa ushirikiano wa pamoja na si waziri mmoja mmoja.

“Mheshimiwa mwenyekiti, sisi (mawaziri) tunafanya kazi kwa pamoja lakini wenzetu (wapinzani) wanapiga kelele pamoja, siyo sahihi kumlaumu mtu kwani hakusimama mezani na kuamua peke yake,” alisema Mwakyembe.

Baada ya kauli hiyo zilizuka kelele kutoka kwa wabunge wa pande zote ndipo Naibu Waziri Manyanya aliposimama na kusema Serikali ina taarifa kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wanaomba rushwa kutoka kwa kampuni na kuwa wanazifanyia kazi ili wakati mwingine wawataje mmoja mmoja.

“Humu ndani Serikali inazo taarifa kuwa baadhi ya wenzetu huko (anaonyesha upande wa upinzani) walikuwa wanaomba rushwa kwa kampuni, tunachunguza na tutawataja,” alisema Manyanya.

Kauli hiyo iliibua mvutano mwingine kwa wapinzani kumtaka Manyanya athibitishe, hata hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliwatuliza wabunge kwa kutishia kuwatoa wengine nje baada ya upinzani kutaka Manyanya afute kauli.

Mbunge wa Tarime Vijijini, Heche alisema mnailinda hii kampuni ya Indo Power Solution akihoji zabuni hiyo ilitangazwa wapi? Nani aliyekuwa anafanya mazungumzo ya awali na kampuni hiyo ambayo gazeti hili la Daily Nation linasema haina hata ofisi Kenya.

“Hivi kama gazeti, mwandishi mmoja anaweza kujua haina ofisi, Serikali inashindwa, gavana, mawaziri watano akiwamo Profesa Palamagamba (Kabudi). Yaani gazeti linaweza kuchunguza kuliko Serikali nzima,” alihoji Heche

“Yaani mtu anakuja hapa anasema alikuja na ndege? Mimi na Esther Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini-Chadema) tunakodi helkopita tunakwenda Tarime kwa hiyo sisi ni wafanyabiashara,” alisema Heche.

Kwa upande wake, Mwambe aliitaka Serikali kuwawajibisha mawaziri wote waliohusika na mkataba huo aliouita ni mbovu na kumwacha Rais John Magufuli afanye kazi au yeye mwenyewe apewe unaibu waziri wa viwanda na biashara kwa kuwa anajua anaweza kufanya kazi hiyo.

Baada ya kauli hiyo, Waziri Mhagama alisimama akiomba utaratibu kuwa suala ambalo Mwambe analizungumza na mawaziri kuwajibishwa limekwisha kutolewa uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge, Chenge hivyo halipaswa kuzungumzwa tena.

Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi (CCM) alimwomba Mwambe kutoendelea kuzungumza hilo kwani mawaziri kama ilivyokwisha kuelezwa wanawajibika pamoja na si mtu mmoja mmoja na kama anataka kuchangia, aielezee Serikali kwa pamoja.

Advertisement