Kenya yabadili noti za Sh1,000

Muktasari:

  • Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Patrick Njoroge amesema noti zote za Sh1,000 zilizokuwa zikitumika zinapaswa kubadilishwa na mpya kufikia Oktoba 1, 2019.

Nairobi. Serikali ya Kenya imechukua hatua ya kukabiliana na watu walioficha majumbani mwao pesa wanazopata kupitia ufisadi na utakatishaji wa fedha kwa kufuta noti ya juu ya Sh1,000 na kuanzisha mpya.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Patrick Njoroge amesema noti zote za Sh1,000 zilizokuwa zikitumika zinapaswa kubadilishwa na mpya kufikia Oktoba 1, 2019.

“CBK (Benki Kuu ya Kenya) imemaliza kutengeneza noti za sura mpya kuambatana na Katiba na sheria zote husika. Noti hizo zilitolewa Ijumaa kupitia kwa tangazo rasmi na sasa ni pesa halali,” alisema Dk Njoroge.

Hii inamaanisha kwamba watakaokosa kubadilisha pesa hizo kufikia tarehe hiyo hawataweza kuzitumia mahali popote kwa sababu zitakuwa haramu.

Dk Njoroge alitoa tangazo hilo siku Rais Uhuru Kenyatta alipozindua noti mpya za sarafu mbalimbali.

Kulingana na gavana huyo, noti za Sh1,000 zimekuwa zikitumiwa na walaghai wanaotengeza pesa feki ambao huhofia kuzipeleka katika benki wakihofia kuchunguzwa na asasi husika za serikali.

Kuficha pesa majumbani hupunguza kusambaa kwa pesa miongoni mwa wananchi na hivyo kutatiza biashara, uwekezaji na hata ustawi wa Taifa.

“Hivi majuzi tumeona noti bandia nchini, hali hiyo imezua hofu kubwa kwani inaweza kutatiza matumizi ya fedha na katika biashara. Ili kukabiliana na hali hiyo, noti zote za zamani za Sh1, 000 zitaondolewa sokoni kufikia Oktoba 1. Wananchi wanastahili kuzibadilisha kwa sababu baada ya siku hiyo hazitakuwa halali,” alisema.

Alifafanua kuwa kabla ya tarehe hiyo, noti hizo zitatumiwa pamoja na zile mpya zilizozinduliwa juzi.

Hatua hiyo itakuwa pigo kwa wananchi wanaoficha pesa nyingi majumbani, hasa wafanyabiashara, wanasiasa na watakatishaji kwa sababu itakuwa vigumu kubadilisha viwango vikubwa vya fedha.

Kulingana na sheria za Kenya, mwananchi yeyote anayechukua au kuweka zaidi ya Sh1 milioni (Sh22 milioni za tanzania) katika benki, huwa anahitajika kujaza fomu maalumu kuelezea zilikotoka au anakozipeleka, anayelipa au kulipwa na kusudi lake.

Mabunda

Katika vita vya kukabiliana na ufisadi vinavyoendelea nchini Kenya a ambavyo Rais Kenyatta aliapa kutolegeza kamba, baadhi ya watu wamekuwa wakipatikana wakihifadhi mabunda ya pesa katika nyumba zao.

Mapema mwaka 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, George Kinoti alisema watuhumiwa wa ufisadi wameficha pesa katika nyumba zao.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa michango mikubwa katika harambee na kuzua maswali kuhusu wanakozitoa.

pesa zote kuanzia kwa sarafu ya Sh50, Sh100, Sh200, Sh500 na Sh1,000 zitakuwa na picha ya Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) na picha za nyati, chui, simba, kifaru na ndovu.

Kila noti inatoa wazo fulani, kwa mfano, noti ya Sh50 inatoa wazo la nishati hai, Sh100 (kilimo), Sh200 (huduma kwa jamii), Sh500 (utalii) na Sh1,000 (usimamizi).

Noti za zamani za Sh50, Sh100, Sh200, Sh500 hazitaondolewa na zitaendelea kutumiwa pamoja na zile mpya. “Itakuwa rahisi kwa vipofu kutumia noti hizo,” alisema Dk Njoroge.