VIDEO: Kesi ya akina Mbowe yasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kupangiwa hakimu

Thursday February 14 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema inasubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa  kuhusu dhamana ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Imesema ikishapata uamuzi huo ndi itapanga hakimu wa kusikiliza kesi yao ya uchochezi.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari 14, 2019 na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ya kufanya mikusanyiko isiyo halali inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

“Naomba kuweka wazi kuwa kesi hii katika mahakama ya Kisutu bado haijapangiwa hakimu yoyote kwa sasa mpaka tutakapopata majalada ya uamuzi kutoka mahakama ya rufaa ndio tutaipangia hakimu wa kuisikiliza,” amesema Mhina.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Wilbard Mashauri ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Awali, wakili wa Serikali, Ester Martin amedai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa.

Wakili wa Utetezi, Profesa Abdallah Safari amedai hawana pingamizi na kwamba rufani iliyokatwa na upande wa mashtaka mahakama ya rufaa itasikilizwa Februari 18, 2019.

Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Novemba 23, 2018 Jaji Mashauri alipokuwa hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya Kisutu alifuta dhamana kwa Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka  masharti ya dhamana.

Baada ya uamuzi huo, washitakiwa hao wanaowakilishwa na wakili Peter Kibatala walikata rufaa mahakama kuu kupinga kufutiwa dhamana.

Hata hivyo, baada ya mahakama kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa Serikali ukiongozwa na mwanasheria, Paul Kadushi amedai kuwa wamekata rufaa katika mahakama hiyo kupinga uamuzi uliotolewa na kuiomba mahakama kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.

Hata hivyo, baada ya upande wa Serikali kuwasilisha rufaa yao,  kuliibuka malumbano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote, huku mawakili wa kina Mbowe wakiongozwa na Kibatala, wakipinga uhalali wa taarifa ya Serikali ya kusudio la kukata rufaa kwa madai hawajafahamishwa na msajili wa mahakama kuu kuhusu kuwepo kwa taarifa hiyo.

Jaji Rumanyika amesema kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa na kwamba kunapokuwepo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.

Jaji Rumanyika amesema mahakama yake imefungwa mikono hivyo anasitisha usikilizwaji wa rufani hiyo hadi hapo itakapotolewa uamuzi katika mahakama ya rufani.

Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Kibamba, Jonh Mnyika; katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi, kufanya  uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka  2018 maeneo ya Dar es Salaam.


Advertisement