Kesi ya kugombea maiti yanguruma hadi usiku

Zuberi Shango Mume wa Marehemu Fatma Kileo mkazi wa Himo Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro,akielekea katika Chumba cha Mahakama ya Hakimu mfawidhi  Moshi mjini,kuskiliza maamuzi ya kesi ya kugombea mwili wa mkewe baada ya ndugu wa mke kufungua kesi ya kutaka Mahakama iwape haki ya kuuzika mwili  huo  kwa dini ya Kikristo badala ya kiislamu Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Pingamizi latupwa, kusikilizwa kesho
  • Uamuzi wa mahakama ulitolewa usiku wakati ambapo upande mmoja ulipoteza pingamizi na hivyo kesi inatarajiwa kuendelea kesho, ilhali hakimu akisisitiza kuwa lazima marehemu atazikwa

Moshi. Kesi ya kugombea mwili wa marehemu Fatuma Kileo (56), kati ya mumewe na ndugu zake, juzi iliendelea hadi usiku kwa Mahakama kusikiliza pingamizi lililowekwa na ndugu hao.

Baada ya shauri hilo lililoanza saa sita mchana na kuendelea hadi saa moja usiku, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernadetha Maziku alitupilia mbali pingamizi la ndugu wa marehemu.

Awali, kesi hiyo ilianza kwa mawakili wa pande hizo kuwasilisha hoja kuhusu pingamizi hilo la kisheria lililowekwa na wajibu maombi; Ausen Nkya na Lodrick Kileo wakitaka kesi hiyo itupwe.

Baada ya kukamilika kwa mabishano saa 9:45 alasiri, Hakimu Maziku aliiahirisha kesi hiyo hadi saa 11:30 jioni ili aweze kuandaa uamuzi, lakini hadi unafika muda huo alikuwa bado hajamaliza.

Mahakama ilirejea saa 12:45 jioni na hakimu huyo alianza kusoma uamuzi wake hadi saa moja usiku na kutupa pingamizi hilo, kisha kueleza kuwa kesi ya msingi itasikilizwa kesho saa 6:30 mchana.

Katika maombi hayo namba 24/2018, Zuberi Shango anayedai kuwa ni mume wa Fatuma anaiomba mahakama hiyo impe haki ya kumzika mkewe baada ya wajibu maombi kumzuia.

Mwombaji huyo kupitia jopo la mawakili wanne; Tumaini Materu, Elia Kiwia, Wilhad Kitaly na Mussa Mziray, anadai alifunga ndoa na Fatuma, Julai 20, 2005 huko Tunduma mkoani Mbeya.

Anadai walifunga ndoa ya Kiislamu na hati yao ni namba 6306 iliyotolewa na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Mbeya (sasa Songwe) na kusimamiwa na Sheikh Idrisa Adeny.

Shango anawalalamikia wajibu maombi kuwa wamemzuia asimzike mkewe kwa hofu kuwa atakuwa na haki ya kurithi mali za marehemu, lakini anadai kuwa hana shida na mali hizo, bali anataka kumzika mkewe.

Uamuzi wa Mahakama

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Maziku alisema moja ya maswali aliyojiuliza ni kama maombi yaliwasilishwa kimakosa na kujiridhisha iwapo ni kesi ya msingi ya kuomba ridhaa ya kuzika.

“Mahakama imeona hakuna kesi nyingine ambayo inaonekana kuendelea baada ya kutoa uamuzi wa maombi hayo. Yaani suala hili halina madai yanayoonekana yataendelea,” alisema Hakimu Maziku katika uamuzi wake.

Alisema, “Hivyo pingamizi lililoweka kuhusiana na kwamba shauri hili halikupaswa kuletwa kama maombi, halina mashiko na mahakama hii inalitupilia mbali.”

Akitoa ufafanuzi wa kifungu cha 95, hakimu huyo alisema katika kifungu hicho hakuna mahali panapoizuia mahakama kutoa uamuzi kwa jambo fulani kwa kuwa kifungu hicho ni cha ujumla.

“Mahakama hii inaona kifungu hiki kinaipa mwanya wa kutoa uamuzi katika jambo lolote maadamu tu haivunji haki,” alisema Hakimu Maziku.

“Nature (asili) ya maombi yaliyoletwa inahusu uamuzi wa ni nani amzike marehemu na hata kama kesi hii itachukua muda mrefu kiasi gani ni lazima muafaka ufikiwe na marehemu azikwe.”

Hakimu huyo alisema, muafaka na uamuzi wa mahakama ni muhimu katika kutenda haki kwenye suala hilo kwa vile maiti hawezi kukaa mochwari milele.

Pingamizi lilivyokuwa

Wajibu maombi kupitia kwa Wakili Godwin Sandi walikuwa wamewasilisha pingamizi la kisheria wakidai kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa kama maombi na kwa kutumia sheria ambayo si sahihi.

Walieleza shauri hilo halikupaswa kufunguliwa kwa njia ya maombi ya dharura bila kuwapo shauri la msingi na kueleza kuwa lilipaswa kufunguliwa kama la kawaida la madai.

Kwa mujibu wa hoja zao, shauri hilo lilipaswa lifunguliwe kwa mujibu wa sheria ya utaratibu wa kuendesha mashauri ya madai sura ya 33 iliyofanyiwa marekebisho 2002, order IV rule (I) naVII (1).

Katika kujenga msingi wa pingamizi lao, wajibu maombi walidai sheria ya uendeshaji mashauri ya madai imeweka utaratibu wa kuyaendesha kama shauri hilo la kugombea maiti.

Jopo la mawakili wa mlalamikaji lilipinga hoja hizo kwa madai kuwa hakuna sheria inayokataza maombi kuletwa kwa namna walivyoyawasilisha na kwamba zipo kesi za mfano ambazo zimeendeshwa kwa utaratibu huo.

Mawakili hao walisisitiza kuwa maombi yao yaliwasilishwa sahihi kisheria, ambayo inairuhusu mahakama kuyasikiliza ili kutenda haki na kuzuia upotoshaji kwani vifungu walivyotumia ni sahihi.

Ndugu kumkana mume

Katika hati ya kiapo kinzani waliyoiwasilisha mahakamani, wajibu maombi, Nkya na Kileo wanasisitiza kuwa Fatuma hakuwahi kuolewa wala hakufia katika Hospitali ya Kilema.

Badala yake, wajibu maombi hao ambao ni ndugu wa marehemu wanadai alifia nyumbani kwake Himo na mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Kilema na ndugu kwa ajili ya kuuhifadhi.

Nkya ambaye ndiye aliyesaini kiapo hicho, anadai hakuna mwana familia aliyewahi kushiriki tukio la kufungwa kwa ndoa inayotajwa na Shango wala hawamfahamu mlalamikaji.

Katika kiapo hicho, ameenda mbali na kueleza kuwa hata watoto watatu wa Fatuma ambao alikuwa akiishi nao katika nyumba yake iliyopo Himo hawakuifahamu ndoa hiyo.

“Marehemu hakuishi na mwombaji (Shango) kabisa. Marehemu aliishi na watoto wake watatu Alex Mollel, Faustin Benard na Getrude Sylvester na hajawahi kuishi maisha ya Kiislamu,” anaeleza Ausen katika kiapo hicho kinzani.

Anasema, “Badala yake (Fatuma) alikuwa Mkristo kama walivyo watoto wake na wakati wote wa maisha yake walikuwa wakienda kanisani na kusali pamoja.”

Mjibu maombi huyo anadai hakuwa peke yake wala na mjibu maombi wa pili (Kileo) katika kumzuia mwombaji (Shango), kuchukua mwili wa marehemu na kumzika kwa imani ya Dini ya Kiislamu.

Badala yake, Kileo anadai kuwa wana familia wa marehemu zaidi ya 100 ndio walioamua kumzika marehemu na yeye binafsi hana sauti katika masuala yanayohusu familia yao kwa vile si kiongozi wa familia.