Hizi hapa sababu za maporomoko ya tope, mbinu za kuyaepuka

Jinsi miundombinu ya maeneo ya mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' mkoani Manyara ilivyoharibiwa na maporomoko ya udongo mwaka jana.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutabairi kuwa huenda kukawa na mvua kuanzia Mei 4 hadi 7, 2024 kwenye mikoa ya Pwani ya Kusini.

Dar es Salaam. Utunzaji wa uoto wa asili kwenye maeneo yenye miinuko mikubwa ni moja ya mbinu zilizotajwa na wataalamu za kupunguza hatari ya kutokea kwa maporomoko ya tope, baada ya mvua nyingi kunyesha.

Kwa mujibu wa wanazuoni waliobobea katika taaluma ya jiolojia na miamba, ingawa matukio hayo si rahisi kuyadhibiti, angalau kuepuka kujenga juu ya miinuko au mabondeni kunaweza kukuepusha na madhara tarajiwa.

Mitazamo ya wasomi hao, inakuja katika kipindi ambacho baadhi ya maeneo nchini yameathiriwa na maporomoko ya tope baada ya mvua zilizonyesha kwa miezi saba mfululizo.

Aprili 14, 2024, shule tano zilifungwa kwa muda na nyumba takriban 20 kuathirika kwa tope lililoporomoka kutoka Mlima Kawetere katika Kata ya Itezi mkoani Mbeya.

Shule hizo ni Tambukareli, Mary’s, Mafanikio, Itezi na Generation kwa mujibu wa Anderson Mwalongo, Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu katika Jiji la Mbeya.


New Content Item (1)
New Content Item (1)


Hali kama hiyo ilitokea wiki na kuongezeka kasi leo katika Mlima wa Kabumbilo kwenda Mwaloni wilayani Muleba mkoani Kagera na kuathiri zaidi ya ekari 10 za mashamba ya wananchi, baada ya kufunikwa na tope hilo.

Taarifa mpya zinasema maporomoko hayo ya tope kutoka Mlima Kabumbilo uliopo katika kijiji cha Ilemela, wilaya ya Muleba mkoani Kagera yamefunika nyumba 13, huku wananchi wakizuiliwa kufika katika eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 29, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amesema nyumba 13 zimefunikwa lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa wala vifo vilivyotokana na maporomoko hayo.

Amesema wananchi wote wamepewa taarifa za kuhama eneo hilo na kwa sasa hakuna mtu anayetakiwa kuendelea kuishi au kwenda eneo hilo maana ni hatarishi.

Amesema wataalamu wanaendelea na uchunguzi wa nini kimetokea.

Kama hiyo haitoshi, wananchi kadhaa walipoteza makazi wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya nyumba zao kufunikwa na tope wiki iliyopita.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wanazuoni wamependekeza kuepuka ujenzi na uendelezaji kwenye mabonde linakokimbilia tope na kwenye milima linakotokea, wakisema hizo ni hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa.


Ni hali inayojirudia

Mwanazuoni wa Uhandisi katika Jiolojia na Utaalamu wa Miamba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kenneth Lupongo anasema kuna uwezekano mkubwa wa matukio hayo kujirudia katika maeneo yaliyotokea.

Uwezekano huo unatokana na eneo lilikotokea tukio hilo mara nyingi hukosa msawazo na inabidi hali ijirudie ili lipate usawa.

“Mara nyingi kwenye eneo lilipotokea huwa linajirudia hadi eneo hilo litakapopata Equilibrium (usawa). Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa tukio kujirudia,” anasema Dk Lupongo.


Maporomoko ya udongo yaliyotokea DR Congo mwaka 2023

Mvua si sababu pekee

Ingawa mvua nyingi ni moja ya sababu za kutokea kwa hali hiyo, mhadhiri huyo anasema zipo sababu nyingine tatu zinazochagiza tukio hilo.

Anazitaja sababu hizo kuwa ni tetemeko la ardhi, milipuko ya volkano na shughuli za binadamu katika maeneo yasiyopaswa, hasa yenye miinuko.

Kuhusu mvua, anasema mmomonyoko huo hutokea pale udongo unapobeba maji mengi na kushindwa kustahimili, hivyo unaporomoka.

Kwa upande wa shughuli za binadamu kwa mujibu wa Dk Lupongo, ni ukataji wa miti na ujenzi, na uendelezaji wa maeneo yasiyopaswa kuendelezwa.

“Matukio haya hutokea kwenye maeneo yenye miinuko mikubwa na kwa Tanzania inajulikana. Maeneo hatari kwa Tanzania ni miinuko ya Usambara, Pale, Kilimanjaro, Meru, Hanang, Uruguru, Mbeya na karibu na mipaka ya Burundi na Rwanda,” anasema.

Anapendekeza kujenga uelewa juu ya uwepo wa matukio kama hayo katika maeneo yenye miinuko ili kukabiliana na hali hiyo.

Anasema iwapo maeneo hayo yatajulikana, itakuwa rahisi kuyafuatilia na kudhibiti hali kabla ya madhara, kwa sababu hayatokei kwa kushtukiza.

“Ni muhimu kujua tabia za maeneo yenye miinuko ili kuepuka kufanya shughuli yoyote au kama inafanywa basi tahadhari ichukuliwe,” anaeleza.


Vigumu kudhibiti

Mtaalamu mwingine wa jiolojia na miamba, Profesa Shukurani Manya anasema ni vigumu kudhibiti hali hiyo katika mazingira ambayo mvua nyingi zimenyesha.

“Maporomoko ya udongo katika miinuko, yanatarajiwa wakati mvua zinapokuwa nyingi na hayadhibitiki. Ardhi ikinyonya maji mengi kuliko kawaida lazima udongo huo ushuke,” anasema.

Lakini, kuna uwezekano wa kupunguza athari za hali hiyo, kwa mujibu wa Profesa Manya.

Anasema hilo litawezekana iwapo uoto wa asili kama vile nyasi na miti inayokuwepo kwenye miinuko hiyo, isikatwe ili kuruhusu maji kunyonywa taratibu.

“Pia, watu wasipende kujenga katika maeneo hayo au chini ya miinuko hiyo na katika njia za mserereko wa udongo ili kupunguza uharibifu wa mali,” anaeleza.


Mbinu kudhibiti

Msisitizo wa mwanazuoni huyo ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, ni kupunguza shughuli za kibinadamu katika sehemu za miinuko na chini yake.

Kufanya hivyo, anasema kutaruhusu uoto wa asili na miti kuota na hivyo kuimarisha kushikiliwa kwa udongo na maji ya mvua kunyonywa taratibu.

Mtazamo wa Profesa Manya unashabihiana na mwanazuoni mwingine katika eneo hilo, Profesa Maboko Makenya aliyesema inawezekana kupunguza ukubwa kwa kuhifadhi mazingira, lakini si kudhibiti kabisa.

Kwa mujibu wa Profesa Makenya, mvua zinapokuwa nyingi na udongo ukatepeta, wakati mwingi hata kama kuna miti ya kutosha inang’olewa na hali hiyo.

“Hii hali ikitokea wakati mwingine inang’oa hadi miamba si miti pekee, kwa hiyo ni muhimu kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kupunguza kiwango cha athari lakini si kudhibiti kabisa,” anasema.

Jambo muhimu, anasema ni wananchi kuhakikisha hawaweki makazi katika maeneo yenye miinuko mikubwa na mabonde kwa kuwa mmomonyoko unapotokea hukimbilia huko.


Viashiria mvua kurudi

Wakati majanga hayo ya kiasiali yakiendelea kujadiliwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema hali ya upepo mkali itaendelea kuwepo hadi Mei mosi, 2024 na huenda ikasababisha mvua kuanzia Mei 4 hadi 7, 2024 kwenye mikoa ya Pwani ya Kusini.

TMA imesema upepo mkali unaoendelea katika maeneo mengi nchini umesababishwa na kuimarika kwa migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo katika ncha ya Kusini mwa Bara la Afrika, ambayo kukoma kwake ndiko kunawezesha mifumo iliyokuwa inaleta mvua kuimarika.

"Hali ya upepo mkali inaenda kukoma ndani ya siku tatu zijazo (kuanzia leo Aprili 29 hadi Mei mosi) na ndiyo itasababisha mvua kurudi kwenye maeneo ya Pwani ya Kusini kuanzia Mei 4 hadi 7," amesema Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla.

Amesema mifumo inaonyesha dalili za mvua kwenye Pwani ya Kusini inayohusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani ambayo ipo jirani na Bahari ya Hindi.

"Kuna signal (viashiria) za mvua zinakuja kwenye mfumo kuanzia Mei 4 hadi 7, tutazitolea maelezo siku zinapokaribia,” amesema.

"Kama nilivyosema, maeneo ya Pwani ya Kusini bado kuna mvua, tunaendelea kufuatilia siku zikikaribia kama mifumo haitabadilika tunaweza kutoa angalizo au tahadhari kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara,” amesema.

"Pia tunafuatilia mifumo kuona kama mvua hiyo itafika hadi Pwani na Dar es Salaam. Kwa sasa kuna viashiria hivyo, siku zitakapokaribia tutatoa taarifa," amesema.

Amesema wakati msimu wa masika ukielekea ukingoni, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua, huku yale ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Dodoma, Singida, Mbeya, Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma mvua ni kama zimeisha.

"Tukiangalia kwenye utabiri zilipaswa kuisha wiki ya pili na ya tatu ya Aprili, lakini hivi sasa kuna misimu miwili inaendelea, ambayo ni ya mvua za msimu zinazoanza Novemba hadi Aprili na za masika zinazoanza Machi hadi Mei,” amesema.

Amesema mikoa inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ikiwamo mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera, mvua zitakwisha kuanzia wiki ya pili hadi ya nne ya Mei.

Wiki iliyopita, TMA ilieleza mifumo inayosababisha viashiria vya mvua kubwa inaenda kudhoofu na vipindi vya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika maeneo mengi nchini zingekoma Aprili 28, 2024.

Kukoma kwa mvua hiyo kubwa kumepunguza adha ya mafuriko katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na maeneo mengine.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa bungeni Dodoma, Aprili 25, 2024  alielezea changamoto za hali ya hewa na kubainisha mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini yaliyosababisha athari kubwa.

Alizitaja athari hizo kuwa ni pamoja na vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli, huku zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 waliathirika.

Watu 155 walifariki dunia na wengine 236 kujeruhiwa kutokana na madhara ya mvua.

Nyumba zaidi ya 10,000 ziliathirika kwa viwango tofauti, miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali ziliathirika.