Kesi ya mfanyakazi wa TRA kuendelea Aprili 9

Muktasari:

  • Kesi ya kushawishi rushwa imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya kwa sababu mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Lilian Wilson amejifungua

Dar es Salaam . Kesi ya kushawishi rushwa inayomkabili ofisa msaidizi wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Joyce Amon (25) itaendelea kusikilizwa Aprili 19, 2019 kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Wakili wa Serikali, Sophia Gura amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Adolf Sachore kuwa kesi hiyo leo Ijumaa Machi 15, 2019 ilipangwa kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Lakini imeshindikana kwa sababu mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Lilian Wilson amejifungua.

Hivyo Hakimu Sachore amesema upande wa mashtaka umebakiza mashahidi wawili wamalize kutoa ushahidi na kufunga kesi yao.

Baada ya kueleza hayo ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 19, 2019 ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi.

Joyce anadaiwa Desemba 12, 2017 katika eneo la Gerezani Kariakoo wilayani Ilala akiwa mwajiriwa wa TRA kama ofisa msaidizi wa kodi alishawishi rushwa ya Sh800,000 kutoka kwa Antelo Sanga ili asiweze kumwandikia cheti cha faini cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Katika shtaka la pili, Lilian Wilson (23) naye anakabiliwa na shtaka la  kusaidia kutenda kosa hilo.

Ilidaiwa kuwa Desemba 13, 2017 katika Hoteli ya Tansome, Lilian alimsaidia Joyce ambaye ni ofisa msaidizi wa kodi wa TRA kujipatia Sh400,000 kutoka kwa Antelo Sanga  ili asiweze kumpatia  cheti cha faini cha VAT.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa walikana na wapo nje kwa dhamana.

Baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua kutoka taasisi zinazotambulika kisheria ambao walisaini ahadi ya Sh5 milioni kwa kila mmoja.