Kikwete: Nilitoa Milioni 30 uwanja wa Simba

Muktasari:

RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amefichua uwanja wa Simba uliopo Bunju yeye ndio ametoa pesa ya kununua.


Dar es Salaam. RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amefichua uwanja wa Simba uliopo Bunju yeye ndio ametoa pesa ya kununua.

Kikwete alisema akiwa Rais wa Tanzania alifuatwa na Mwenyekiti wa zamani Simba, Alhaji Aden Rage na kumwambia wamekwama Milion 30 za kununua uwanja na aliwaambia wamepata.

"Ukiwa kiongozi inabidi uwe unatoa kwa hiyo mimi nilifuatwa na kuambiwa na nikatoa, lakini sisemi haya kwa kuwadai wala kukumbushia labda. Lakini pia nasema hili kukuomba Waziri Mkuu nawe uchange na umfikishie Rais naye achange,” alisema Kikwete.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga kutokuwa wanyonge hasa katika kipindi hiki ambacho Watani wao Simba wamekuwa wakifanya vizuri.

"Wanachama wa Yanga inabidi muwe na hisia na timu yenu, sasa hivi hata jukwaani hamshangilii yaani tofauti na Simba ambavyo nawaona wakiwa jukwaani,” alisisitiza Rais Kikwete.

Aliongeza licha ya kutokuwa Mwenyekiti wa Yanga wala katika kamati ya usajili katika klabu hiyo amekuwa akihusika katika usajili ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.

UONGOZI WAPEWA NENO

Wakati huohuo Kikwete aliupongeza uongozi mpya wa Yanga  huku akiwataka viongozi hao wafanye mabadiliko katika timu hiyo.

"Kuna kipindi nilipata tabu sana. Yanga ni klabu ya wanachama lakini imepoa nikikumbuka mimi nikiwa mdogo wanachama walikuwa wanakutana pale klabuni na kutoa mawazo na kufanyiwa kazi.

Nawaomba Msolla na wenzako. Tunawategemea na timu yenu ni nzuri na mmechagua watu ambao wanaujua mchezo wa mpira tofauti na watu ambao wanatafuta uongozi kwa ajili ya kupata umaarufu.

"Kuna watu wakishinda wanalala usingizi, wakifungwa wana lala usingizi huyo sio kiongozi wa Yanga," alisema Kikwete.

Aliushauri Uongozi huo uongozi wa Yanga kuwekeza katika soka la vijana kwani klabu yao ina historia ya kukuza soka la vijana.