Kilichojificha nyuma ya nywele bandia

Moja kati ya urembo ambao wanawake wengi Wakitanzania wameupa kipaumbele ni pamoja muonekano wa nywele wawapo kazini, bungeni, kwenye sherehe na hata nyumbani.

Japo baadhi ya watu hudai kuwa uzuri wa mwanamke umefichwa ndani ya nafsi, lakini muonekano wa nje hasa wa mavazi na nywele hubeba tafsiri ya mtu anapopita katikati ya watu.

Wakati wataalamu wa afya wakieleza nywele bandia zinazovaliwa kichwani kama kofia na kugundishwa na gundi yake maalumu, zina athari kiafya, hivi karibuni Serikali imependekeza kutoza ushuru kwenye nywele hizo zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Akiwa bungeni wakati akisoma bajeti ya mwaka 2019/20, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema; “Napendekeza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele bandia zinazotengenezwa nchini na asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali.”

Ni wazi kuwa siku hizi kumeibuka suala la kubandika nywele hizo maarufu kama ‘kubond’ kwa kutumia gundi na kuonekana kuchangamkiwa vilivyo na wanawake kwa kuwa humfanya aonekana ana nywele kama za asili ya Kizungu.

Suala hilo limekuwa likifanywa bila kujali madhara ya ngozi ya kichwa au afya ya nywele zao.

Mmoja wa wanawake hao, Jessica Shunzu aliyekutwa anabandika nywele kwa gundi, anasema hiyo ni njia rahisi kwake kwa sababu anaogopa kuchomwa na sindano wakati wa kuzishonea kichwani.

“Mimi ni muoga sana, hivyo hii njia ni rahisi kwa sababu nabandika bila maumivu na sikai chini muda mrefu kusubiri kushonewa,” anasema Shunzu.

Mmiliki wa saluni eneo la Mtoni Kijichi, Jamilah Jailaji anasema zipo aina tofauti za kubandika nywele kwa wateja kwa kutumia gundi kutegemea na chaguo lake.

“Aina ya kwanza ni kubandika nywele hizo juu ya kofia ndogo za kulalia zisizokuwa na matundu kwa mtindo anaohitaji mteja, lakini ya pili ni ile ya kubandika katika ngozi moja kwa moja ili iweze kushika vizuri. Baadhi huwa wanahisi kama wakibandika katika kofia inaweza kuvuka wakati wa purukushani mbalimbali hasa watumiaji wa daladala, hivyo wanaona kutumia gundi katika ngozi ni bora zaidi.

“Wakati wa kubandika wigi huwa najitahidi sana niweke katika ngozi nisiguse nywele ili hata mteja akiamua kutoa nyumbani asiharibu nywele zake kwa sababu huwa tunawashauri angalau wakae nazo kwa wiki moja,” anasema Jailaji.

Anasema katika kubandika mawigi hayo, zipo bei tofauti kulingana na chaguo la mteja na bei huanzia Sh15,000 kwa wigi fupi hadi Sh100,000 kwa yaliyo marefu zaidi.

Hiyo ni gharama tofauti na bei ya kununua wigi dukani ambayo yale mazuri na yanayopendwa zaidi huuzwa kuanzia Sh300,000 hadi 1,000,000 kutegemea na unalotaka.

“Baada ya kukaa nazo kwa muda na mteja akiwa anahitaji kutoa wigi hilo nyumbani, anashauriwa kutumia dawa ya kutoa rangi kwenye kucha ‘remover’ au ‘steaming.”

Mmoja wa watu wasiopenda kutumia nywele bandia, Anna Lindu anasema kutojiamini kwa wanawake ndiyo kunawafanya kutumia njia mbalimbali za kuongeza urembo kwa kufanya vitu vinavyoweza kuwaletea madhara.

“Nibandike nywele ili iwaje? Kiukweli kuongeza ongeza vitu kichwani na joto hili mimi siwezi. Sasa unatumia gundi kuweka katika ngozi hatujui zinashida gani, zimetengenezwa kwa kutumia nini hatujui ila tunapenda kuiga tu mambo kutoka nje,” anasema Lindu.

Wanaume wanasemaje?

Ally Hassan, mkazi wa Magomeni anasema haelewi ni kwa sababu gani wanawake huwa wanahangaika kuongeza nywele bandia kichwani ili kuwavutia watu wengine. “Nikuambie kitu, sisi wanaume hatupendi wanawake wenye mambo mengi, wakati mwingine hawa wanaoweka hayo madude (nywele bandia) huwezi kukaa nao karibu yanatoa harufu (kunuka jasho), wengine hawayachani,” anasema Hassan.

Mwanaume mwingine, Rashid Msakuzi anasema mamlaka zinazohusika kuthibitisha ubora ni lazima zihakiki bidhaa zote zinazotumiwa katika mwili wa binadamu kabla ya kufika kwa watumiaji hasa gundi wanazobandika nywele kichwani ili kufanya Taifa kuwa salama.

“Najua (mamlaka husika) wanahakiki, lakini ni vyema hata zile njia za panya zinazoingiza bidhaa hizi zidhibitiwe ili kuhakikisha vitu vinavyotumika visiwe na matokeo hasi baadaye maana hatuna namna tunayoweza kufanya wanawake wasifanye urembo wao.

“Na siyo kwamba (wanawake) hawajui madhara wanayoweza kuyapata, bali wanadharau kwa sababu magonjwa mengine hutumia muda mrefu kuwapata watu ndiyo maana huwa wanajipa moyo,” anasema Msakuzi.

Thomas Andrea anasema uzuri wa mwanamke haupo katika kuongeza vitu vya bandia bali kupitia uhalisia wake huku akibainisha kufanya hivyo ni kutokujiamini.

“Ukimuweka mwanamke aliyekata nywele na aliyeweka nywele bandia yule aliyekuwa na uasilia atapendwa sana na wanaume kuliko huyo asiyejiamini na alivvyoumbwa, sisi hatupendi watu wenye mambo mengi,” anasema Andrea.

Wataalamu wa afya wanasemaje?

Daktari wa binadamu, Samwel Shita anasema ubandikaji wa nywele bandia kwa kutumia gundi huweza kusababisha mzio kwa muhusika kutokana na aina ya kemikali zilizotumika katika utengenezaji wa gundi hiyo.

“Mzio huo husababishia vipele na muwasho kwa sababu siyo kila kitu kinaweza kuwa salama kwa ngozi, vingine siyo rafiki kwa ngozi ya muhusika. Japokuwa vingi vinavyoingizwa nchini vinaonekana ni salama lakini kuna watu wanaotumia njia za panya kuleta bidhaa hizo sasa zinaweza kuleta shida mbalimbali kwa watu,”anasema Dk Shita.

Pia, anasema mbali na uzio madhara mengine ni mhusika kupata michubuko wakati wa ubanduaji nywele hizo.

Daktari wa binadamu, John Haule anasema wanawake wengi hufanya vitu vya urembo katika miili yao bila kuangalia madhara yatakayowapata baadaye.

“Unaweza kutokwa na vipele kichwani na kujikuna… na hii huweza kusababisha muhusika ahangaike kutumia dawa nyingi bila kufahamu kama shida ni gundi hizo ambazo pia zinaweza kusababisha saratani ya ngozi na hata damu.

“Unapofunika kichwa kwa kugandisha nywele za bandia na gundi zaidi ya wiki, kichwa kinapata mba ambao watasababisha muwasho mkali kwa muhusika, unaoweza kumpa maumivu kichwani baada ya kujikuna kwa muda mrefu lakini mba hao huweza kuingia ndani ya mwilini kupitia damu.

“Wakiingia mwilini (mba) ndiyo hapa utakuta mtu anaumwa magonjwa ya ngozi, maambukizi ya wadudu katika damu na hajui haya yote ameyapata wapi,” anasema.

Ushauri

Hata hivyo, Dk Haule anawashauri wanawake kutumia njia bora katika urembo hasa zile zinazoweza kuruhusu nywele halisi ‘kupigwa’ na hewa.

“Hata kama anavaa mawigi basi akumbuke kusafisha nywele zake mara kwa mara na kupaka mafuta katika ngozi ili kuepusha ukavu wa ngozi na mba wanaoweza kumpata,” anasema Dk Haule.

Theresia Maganga (70) anasema zamani kulikuwa hakuna ubandikaji wa nywele bandia wala kuongeza nywele katika kichwa bali ilikuwapo njia ya kufanya nywele ya asili kuvutia zaidi.

“Tulikuwa tunatumia bati, linatobolewa matundu na msumari; nywele zinapakwa mafuta mengi sana, lile bati linawekwa motoni hadi lipate moto.

“Kisha (watu wa nyumbani au saluni) wanaanza kulipitisha bati katika nywele kwa uangalifu ili wasije kukuunguza masikio na kwenye paji la uso au unaweza kuziba sehemu hizo kwa kujifunga kitambaa kizito.

“Baada ya hapo nywele zinakuwa kama zimewekwa dawa, laini na hii ilikuwa ikitumika hata kwa mabibi harusi na wakati mwingine walikuwa wanasukwa ulalo (nywele za mbenjuo) zinazopasua kichwa,” anasema Maganga.