VIDEO: Kituo cha majaribio ya utoaji dawa ya usingizi chazinduliwa

Muktasari:

  • Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia katika vifaa vya tiba ya nchini Marekani, pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) wamezindua kituo cha kwanza Tanzania cha kufanyia majaribio katika utoaji dawa za usingizi na uokoaji wa maisha

Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia katika vifaa vya tiba, Gradian Health Systems ya nchini Marekani, pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) wamezindua kituo cha kwanza Tanzania cha kufanyia majaribio katika utoaji dawa za usingizi na uokoaji wa maisha kwa wagonjwa wa dharura.

Lengo la ujio wa kituo hicho cha kisasa na kitakachotumia vifaa vya teknolojia rahisi kwa mazingira ya Kitanzania ni kuboresha utoaji tiba kwa wagonjwa walioko katika dharura wakati wa upasuaji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho leo Jumapili Aprili 7, 2019, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema Serikali inafanya yote hayo kuhakikisha huduma ya kumtoa mama mtoto tumboni na huduma nyingine za upasuaji zinafanywa na watu wenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma.

Amesema asilimia tatu ya vifo vya kina mama wanaofariki katika uzazi vinatokana na kukosa huduma bora za dawa ya usingizi, hivyo wanataka kuhakikisha wanapunguza vifo hivyo kwa asilimia kubwa.

 “Imani yetu ni kuwa hawa wanaopata mafunzo hapa wakitoka watakwenda kufanya kazi ipasavyo maeneo wanayotoka, huu ni utaratibu wa kawaida hata ndege zinapoagizwa marubani hupelekwa kwa ajili ya kupata mafunzo kwanza kabla ya kuanza kufanya kazi,” amesema Dk Ndugulile.

Kwa upande wake  Rais wa Chama cha  madaktari bingwa wa kutoa dawa za usingizi na maumivu (Sata) Dk Mpoki Ulisubyisye amesema changamoto kubwa ni ujuzi wa kutumia vifaa vilivyopo hivyo madaktari wanapaswa kupata mafunzo ya namna ya kuvitumia.

Amesema  vifaa hivyo vya kutolea dawa za usingizi (Universal Anesthesia Machine-UAM), havitumii umeme wa gridi na hujitengenezea hewa ya Oksijen vyenyewe, hivyo, vinafaa kwa vituo vya kutolea huduma ambavyo vinakumbana na changamoto ya kukosekana kwa umeme na upatikanaji wa gesi ya Oksijeni ya kununua (kwa ajili ya tiba).