Kosa la Hamisa, Uwoya ni pacha

Saturday May 25 2019

Hamisa, Uwoya, sanaa, muziki, video, diamond, WCB, wasafi, zari, Mange, mwanaharakati,

 

By Dk Levy

Mrembo sana. Ni vigumu kuelezea kupitia maandiko haya ukapata picha kamili. Omba upate nafasi kuonana naye. Maana kuna wanawake bila maombi na funga ya siku 40 kutokula na kunywa. Huwezi si tu kumpata bali hata kumuona kwa mbali. Huyu mrembo ni mmojawapo, hawezi kuishi nchi moja na Gigy Money.

Sisi wengine tulipigwa talaka na malaika wanaotoa pesa kama za Mo Dewji. Lakini wale malaika wa kwenye mbavu za Samson hata akapata wasaa wa kummiliki Delila, hao nasi tunao. Naamini Samson mwenyewe kama kwa Delila wake tu alinyoa rasta. Kwa Delila wangu huyu angejikata na shingo lote. Jilazimishe kuamini kuwa nilikuwa na kiumbe wa ajabu haijapata kutokea.

Nina vipaji vingi. Mojawapo ni kipaji bora zaidi cha kutambua urembo wa mwanamke. Huyu alikuwa mrembo kiasi hata kipaji changu cha kutambua warembo kilishangaa kutambua urembo wake. Hana mfano duniani. Ombeni nife na kufufuka pengine mfano wake nitaupata peponi ili nije kuwasimulia.

Duniani wanawake ni wengi kuliko wanaume. Lakini wanaume ni wengi zaidi walio ‘aktivu’ kuliko wanawake. Wakati mwanaume anaweza kuamua chochote. Mwanamke hupangiwa ratiba na matakwa yake na bwana au maumbile yake. Anaweza kuahirisha kikao kizito kwa sababu hana nywele mpya. Hana pamba mpya au hana simu mpya.

Ama bwanaake ‘kamchiti’ au kamjibu hovyo jana yake basi kwa hiyo hana ‘mood’. Yaani jambo dogo tu linaweza kukwamisha mishemishe za dem.

Namuona malaika tuliyepanga miadi ya kufanya naye ujinga. Kapaki gari ya hadhi akipiga hatua kuufuata mlango wa pepo yake ya siku hiyo. Maana pamoja na urembo wake wa ajabu, naye alikuwa na bahati ya pekee kukutana nami nikiwa kwenye umbile la kibinadamu toka kwenye tumbo la Mama Levy.

Advertisement

Nilivuta pumzi ya hofu na furaha. Hata Trump na Dangote akikutana na dem huyu lazima avute pumzi niliyovuta. Haraka sana nikaenda kujitazama kwenye kioo kilichopo kwenye kabati kubwa ndani ya chumba. “Mbona huulizi kwa nini nasaliti ndoa yangu?” Ni swali la Sophia akiwa kando yangu akinipapasa ingawa mpaka sasa sikumbuki ni eneo gani la mwili alilopapasa. Kifupi ni baada ya kumfanyia ufundi mwingi niliyojaaliwa bila kupitia Veta. Sina hakika kama nilimjibu ingawa naye hakutaka kusubiri jibu langu zaidi ya kunieleza matatizo mengi ya ndoa yake ambayo pia niliyapuuza.

Kuna wakati binadamu huhitaji kusikia matatizo zaidi ya furaha. Ndio hali niliyokuwa nayo. Sikutaka kupoteza pointi mwisho nionekane mwanaume mwenye makazi Kinondoni. Wakati ukweli mimi mwenyeji wa Ikwiriri na Maneromango. Kwanza mara ya mwisho kwenda Kinondoni ilikuwa wakati ule wa Vinega wa Anti Virus viwanja vya Ustawi wa Jamii miaka 9 iliyopita.

Kuna wanawake akilala anavutia, akisimama anavutia. Akitembea anavutia akicheka anavutia. Akilia anavutia hata akikutukana anavutia. Ndo huyu, hata ukimkuta anamroga mkeo atakuvutia tu.

Video ikanihamisha toka kwenye dunia ya mahaba mujarabu, mpaka kwenye hisia kali juu ya wasanii na sanaa. Kuna wingu zito limetanda mbele ya nyuso za wasanii wa muziki na filamu linalopelekea kazi ya sanaa iwe ngumu kuliko ugumu wenyewe. Sasa haijulikani alaumiwe nani. Wasanii, Basata, mameneja, mashabiki au mvua zinazonyesha?

Nakunong’oneza mwaka 1991, kabla Whitney Houston hajaolewa na Bobby Brown, baba yake Whitney, John Russell Houston Jr alidata na mafanikio ya MC Hammer, akamfuata bila aibu na kumuomba amuoe binti yake, yaani Whitney, ombi ambalo halikuwezekana. MC Hammer alikuwa juu si tu ndani ya Marekani mpaka Kakola huko Geita.

Msanii usiwafanyie fujo wenzako kwa kuwa una nyumba Daslama mjini. MC Hammer alitumia dola 30 milioni, sawa na Sh63 bilioni za sasa kwa ujenzi wa nyumba yake, huko Fremont, California. Ikiwa na ukubwa wa futi za mraba 40,000.

Alikuwa na watumishi 200 waliolipwa mshahara na posho. Mishahara yao iligharimu dola 6.8 milioni kila mwaka, Sh14.7 bilioni ya sasa hivi.

Aliingiza fedha nyingi sawa sawa na matumizi ya fujo nyingi. Ni binadamu wachache walioonja ladha ya nusu pepo wakiwa duniani. Watu wanamuona Floyd Mayweather Jr kuwa mkali wa matanuzi, huyo ni mwanafunzi wa chekechea kwa MC Hammer. Mwenye fedha zake alijua kuzitumia.

MC Hammer alikuwa bonge la dansa. Alikuwa anagonga shoo zenye kiwango cha juu. Alifanya muziki uende kwenye njia zake. Ubunifu wake wa kuchanganya Rap na Pop ulimfanya awe mwanamuziki lulu. Alivuna sifa alizostahili, ingawa kuvuma kwake kulikoma mapema. Jamaa alitengeneza fedha nyingi lakini muziki ulipogoma kumuingiza pesa kila kitu kiligeuka juu chini.

Haya maisha yapo kwa wasanii wa sanaa zote nchini. Wana uwezo mkubwa wa kufikiri pale wanapopambana kutoka kisanii ili wawe mastaa. Lakini umaarufu wao kadri unavyoongezeka ndivyo uwezo wa kufikiri unavyotoweka. Wanaanza kujilazimisha kuishi sawa na ukubwa wa majina yao wakati pesa wanayoingiza ni tofauti na umaarufu wao.

Umaarufu hugeuka mateso. Na utumwa wa maisha yao. Wengi hujikuta Jay Z au Anjelina Jolie kwa kipato cha mwalimu wa Sayansikimu pale Usililojua Primary School. Nini hutokea? Kupanga nyumba kubwa na kushindwa kujenga. Kujipigisha picha na pamba za promo kwa kupost insta. Na hata wenye madanga amazing toka ‘Ikulu ya Nairobi’ wako ‘bize’ na ‘shoo ofu’ kuliko miradi.

Wanaodanganya kujenga wakati kapanga ni matokeo ya mateso ya utumwa wa kistaa, wanaamini staa anatakiwa aishi usawa wa njia ya kwenda Bagamoyo. Ndo maana hata kama ana nyumba nzuri Keko, lakini kapanga jumba kubwa Mbezi tofauti na hitaji la makazi yake utadhani ubora wa kazi zake hutokana na madimbwi ya maji ya Mbezi na Mbweni.

Ni kama wanaambukizana kizazi na kizazi. Wa mwanzoni mwa miaka ya 2000, mizuka yao ilikuwa kwenye ‘mabaluni’ na kuchafua meza baa. Nyumba haikuwa dili saana kwao. Hawa wa 2010 kuja juu mabalaa yao yapo kwenye kupanga majumba ya gharama na kumiliki madem au mabwana wengi kuliko kelele za vyura pale Jangwani.

Wenye kutumia vyema umaarufu kwa kuwekeza wapo. Lakini idadi yao ni ndogo kulinganisha na wanaotengeneza umaarufu mkubwa sawa na umasikini mkubwa. Wanatumia nguvu na pesa nyingi kuishi kistaa kuliko uwezo wa kutengeneza pesa za ustaa. Nchi inaonekana inazalisha majina makubwa ya vijana wenye umasikini mkubwa kwa upuuzi wao wenyewe.

Kosa la Wema, Hamisa, Uwoya ni lile lile la V-money. Badala ya shabiki kumfuatilia staa, hivi sasa staa ndo humfuatilia shabiki. Yaani wanaishi kwa kumtazama shabiki badala ya shabiki kumtazama staa. Wakati wenzetu ni vigumu kuona staa anajibishana na shabiki mitandaoni. Bongo yetu staa kutukanana na shabiki mitandaoni ni kawaida kama kuchokonoa meno baada ya kula ndafu.

Siku wakiacha kuishi kwa kumtazama shabiki watapiga hatua. Wataacha kuishi kwa kuigiza ili kuwakomoa mashabiki. Hawata danga ili wapate pesa ya wigi jipya kila wiki. Watakuwa huru kupanga maisha yao kwa msingi wa kibinadamu badala ya hivi sasa wanavyolazimisha kuwa Beyonce wa mitaa ya Sinza. Wanajiumiza bila sababu ya msingi.

Kwa maisha ya Kibongo hawa mastaa wanachopata ni kingi ingawa sicho wanachostahili. Tatizo wanashindwa kutunza wanachopata kama wanavyotunza namba za simu za madingirai au totoz za mjini. Sihitaji kuwa staa ili nimiliki totoz kali mjini. Bali nahitaji mkwanja ili niitengeneze totoz yangu iwe kali mjini. Mastaa wetu wanakwama wapi?

Manaake ni kwamba matukio yenu ya kila siku ni rafiki kwa macho na masikio ya mashabiki wenu kuliko uongo wenu wa kwenye filamu. Shitukeni. Ni vigumu watu kuwa na hamu na wewe au kazi yako. Wanajisifia kuwa magazeti ya udaku siku hizi hayana soko kwa sababu kila kitu kipo Instagram.

Sawa ni kweli ila Instagram inakusaidia nini? Kama una wafuasi milioni mbili halafu kazi yako ya filamu huwezi kuuza hata kopi 500 mtaani? Si kichaa hicho? Unafurahia likes na comments tu. Una wafuasi mamilioni mitandaoni ukurasa wako hauna tangazo hata moja la biashara linalokuingizia pesa.

Miaka ya karibuni wanakimbilia kwa ‘watumishi’, maaskofu na wachungaji kuombewa. Kinachowapeleka wengi wao ni kupata mume, ndoa au mimba. Haya nd’o matatizo ya dada zetu. Na matatizo haya umekuwa mtaji kwa makanisa mengi ya kiroho.

Nataka kumaanisha nini? Kwamba kisiwe kitu cha ajabu watumishi kukutwa na janga kama hili. Na huyu amekuwa mhanga wa ‘skendo’ hizi kwa sababu si mara ya kwanza. Huwezi kuvuna njegere kwenye shamba ulilopanda kunde. Waumini wao wengi ni kinamama.

Jitu linaendekeza mipombe, bange na kila aina ya ulevi kiasi linashindwa kutimiza wajibu wake kwa mkewe.

Mwanamke anajua karogwa nd’o maana hapati mimba anaamua kwenda kwa watumishi wamuombee. Kumbe hana tatizo lolote bali mume ndiye anayehitaji maombezi.

Advertisement