Krismasi Moshi kwa treni mwaka huu

Muktasari:

  • Kadogosa alisema mbali na mizigo, pia wamekuwa wakishuhudia abiria wengi wa mikoa hiyo wanavyopata tabu kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka, hivyo lengo lao ni ifikapo Desemba mwaka huu treni katika njia hiyo iwe imeanza kufanya kazi.

Kibaha. Ile adha wanayoipata wakazi wa mikoa ya Kaskazini ya tabu ya usafirikatika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka huenda mwaka huu zikafika ukingoni baada ya usafiri wa treni kuanza.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mikakati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufufua reli ya ukanda huo wakati wa ziara ya wasanii kutembelea ujenzi Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) juzi, mkurugenzi wa shirika hilo, Masanja Kadogosa alisema mwekezaji waliompa kazi ya kusimamia njia hiyo alifanya makosa kuifunga kwani ina umuhimu katika uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja

Alitoa mfano kuwa, kwa sasa saruji nyingi inayozalishwa katika kiwanda cha Simba jijini Dar es Salaam soko lake kubwa ni mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

“Uwapo wa kiwanda hiki cha simenti (saruji) ni hitaji tosha la usafiri wa treni kurudi kwani mbali na kupunguza gharama itasaidia barabara zetu zidumu muda mrefu na fedha za kuzikarabati kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo,” alisema.

Kadogosa alisema mbali na mizigo, pia wamekuwa wakishuhudia abiria wengi wa mikoa hiyo wanavyopata tabu kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka, hivyo lengo lao ni ifikapo Desemba mwaka huu treni katika njia hiyo iwe imeanza kufanya kazi.

“Mkandarasi yupo site (eneo la ujenzi) na ameshafika maeneo ya Same,” alisema.

Akizungumzia usafiri wa treni ndani ya jiji la Dar es Salaam, Kadogosa alisema wanatarajia kuleta treni za kisasa na kuondoa zilizopo na njia zitaongezwa.

Naye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alikuwapo katika ziara hiyo aliwataka wasanii kuwapuuza wanaowabeza kuwa wamenunuliwa ili kufanya ziara hiyo na kuwataka kuwa mabalozi wa kutangaza mandeleo hayo.

Mratibu wa ziara hiyo, Steven Mengere (Steve Nyerere) alisema kwa kile walichojionea watakwenda kutangaza maendeleo hayo kwa kutengeneza makala maalum.