UCHOKOZI WA EDO: Kuna wadaiwa sugu na wengine watazamaji sugu

Monday June 24 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Nchi hii bwana! Watu wanapiga pesa kimya kimya huku maskini akiwa hajui. Yaani ni mwendo wa kimya kimya. Majuzi tukaletewa majina ya wadaiwa sugu wa mikopo fulani hivi una jina la Kiingereza. Mara nyingi pesa hazitoki kwa miradi yenye jina la Kiswahili.

Pesa nyingi kama zile za EPA huwa zina majina ya Kiingereza zaidi. Hauwezi kukuta miradi mikubwa yenye maneno ya Kiswahili. Mradi wa juzi ambao wanadaiwa watu wamepiga pesa unaitwa Commodity Import Support. Tulioishia darasa la saba huwa tunaona nyota tu tukitajiwa viingereza hivi.

Nimeona kuna majina ya wanasiasa maarufu pale. Kuna majina ya wafanyabiashara maarufu pia. Kuna mzee wangu mmoja pale nadhani ile sura yake wanaogopa hata kwenda kumdai. Anaweza kurusha ngumi. ‘anyway’ Kinachotuacha hoi sisi maskini ni jinsi ambavyo tunaletewa kesi kama hizi wakati watu walishapiga pesa za kutosha.

Hauwezi kusikia mikopo kama hii wakati inaanzishwa. Mara nyingi tunasikia wakati wa kesi au wakati wa kutajana majina ya wadaiwa. Kuna wajanja wanaidaka juu kwa juu, wanaipiga juu kwa juu, sisi maskini tunabakia kuwa mashahidi wa kesi. Kazi yetu ni kuweka mkono shavuni na kusikiliza kesi tu.

Zamani wakati wa Bunge la utawala uliopita tulikuwa tunashuhudia kesi hizi kama mechi za soka. Watu tunajaa vibanda umiza kuwasikiliza akina Zitto wakicharurana na watuhumiwa ambao wengine walikuwa ndani ya Bunge. Siku hizi hakuna habari ya Bunge live kwa hiyo tunaletewa kesi katika jamii kama hii ya juzi.

Ujumbe wangu ni kwamba siku nyingine mtutangazie hii mikopo kabla haijakopwa. Tabia ya kupeana pesa kwa siri siri halafu kesi tunaletewa wananchi tumechoka. Kwa mfano, pesa hizi zimetuumiza walalahoi kwa sababu kumbe mkopo wake ulikuwa hauna riba.

Advertisement

Yaani matajiri wanajua namna ya kunasa hizi dili nyepesi ambazo zinawafanya wawe matajiri zaidi huku walalahoi wakiteseka na mikopo yenye riba kubwa.

Siku nyingine tushtuane mapema kuliko kuletewa kesi mezani. Tumechoka kuwa watazamaji sugu. Na sisi tunatamani siku moja tuwe wadaiwa sugu.

Advertisement