Lema: Nitajiuzulu ubunge Ndugai akithibitisha Lissu amelipwa fedha za matibabu

Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kushoto) akizungumza na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema ndani ya Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma

Muktasari:

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema ikiwa Spika wa Bunge, Job Ndugai atathibitisha kuwa Tundu Lissu amelipwa fedha kwa ajili ya matibabu, atajiuzulu ubunge 

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema ikiwa Spika wa Bunge, Job Ndugai atathibitisha kuwa Tundu Lissu amelipwa fedha kwa ajili ya matibabu, atajiuzulu ubunge.

Leo Alhamisi Januari 31, 2019 bungeni jijini Dodoma Ndugai amesema hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alikuwa amelipwa Sh207.8milioni.

Amesema pia mwanasheria mkuu huyo wa Chadema alilipwa Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake, kwamba jumla ya fedha alizolipwa ni Sh250milioni.

Ndugai amesema leo kuwa mbunge huyo amekuwa akilalamika kila wakati kuwa Bunge halimjali kitu ambacho hakina ukweli ndani yake na hakuna madai kama hayo.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter Lema ameandika, “Bunge halijawahi kumlipia Lissu pesa kwa ajili ya matibabu. Alichokisema Ndugai ni upotoshaji kwa jamii na Mungu. Chama kitatoa yamko la juu hili. Spika akiweza kuthibitisha hili, mimi najiuzulu ubunge. Mshahara wa mbunge sio hisani ya Spika.”