Ndugai: Lissu amelipwa Sh250milioni kutoka bungeni
Muktasari:
Spika Job Ndugai amesema yupo tayari kuanza kumjibu mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), kwa maelezo kuwa mwanasheria mkuu huyo wa Chadema sasa amepona
Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema kuanzia sasa ataanza kumjibu mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kwa kuwa ana amini amepona na kwamba tayari ameshalipwa Sh250milioni kutoka bungeni.
Ndugai ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 31, 2019 bungeni mjini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Amesema hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu ya mbunge huyo.
Amesema kwa ujumla hadi sasa Lissu amelipwa Sh250milioni kutoka bungeni.
“Siku za mwanzo sikutaka kujibu maana niliamini kumjibu mtu aliyelala kitandani siyo vizuri kwani kuna vitu huenda vingekuwa vimempita, lakini sasa naamini ni mzima hadi anafanya ziara nje. Nalisema hili akijibu nakuja na mkeka hapa,” amesema Ndugai.
Amesema mbunge huyo amekuwa akilalamika kila wakati kuwa Bunge halimjali kitu ambacho hakina ukweli ndani yake na hakuna madai kama hayo.