Lema amjibu Spika Ndugai kuhusu deni

Dar/Dodoma. Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akitangaza bungeni deni ambalo Godbless Lema anadaiwa na kwamba ndio chanzo cha msongo wa mawazo kwa mbunge huyo wa Arusha Mjini (Chadema), mwenyewe amesema si kosa kwake kudaiwa na bado ataendelea kukopa.

Lema alisema hayo jana muda mfupi baada ya Bunge kupitisha azimio la kumsimamisha mikutano mitatu kuanzia huu wa bajeti Januari au Februari mwakani.

Mbunge huyo ameadhibiwa kutokana na kuunga mkono kauli iliyotolewa na mbunge mwenzake wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) kuwa Bunge ni dhaifu ambaye naye amesimamishwa vikao viwili.

Lema akizungumza na Mwananchi jana kuhusu uamuzi wa Spika Ndugai kutangaza deni analodaiwa na kwamba linaweza kuwa sababu ya mbunge huyo kuwa na msongo wa mawazo, alisema si kweli na kukopa si dhambi.

“Maana nyinyi (wabunge)ni wawakilishi wa wananchi unapokuja hapa lazima uwakumbuke watu waliokutuma hapa. Ukitanguliza person interest (maslahi binafsi), ukisema mimi siogopi, sio wewe, wale wana haki (wapiga kura) lazima upime kati ya wale na wewe.”

“Yapo mambo ambayo hawasemi wacha tuseme kidogo, amekopa Sh644 milioni, sasa hivi amelipa zimebaki Sh419 milioni huu ni msongo wa mawazo ndio maana anafika mahali anajilipua tu nakadhalika,” alisema Ndugai wakati akitangaza deni la Lema.

Jana, Lema alisema: “Spika kama alifikiri ananidhalilisha hajafanikiwa kwani mimi kudaiwa sio dhambi na nitaendelea kukopa.”

“Hata jengo la Bunge likiwa linakopeshwa nitalikopa, kwani sijawahi kushindwa kulipa, wabunge wengi wana mikopo hata Spika mwenyewe anaweza kuwa anadaiwa lakini kama hadaiwi basi ni yeye,” alisema.

Kuhusu kauli ya Ndugai kuwa ana msongo wa mawazo, mbunge huyo alisema: “Hili nawaachia wananchi wapime kati yangu na Spika Ndugai nani mwenye msongo wa mawazo.”

Lema anaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk James Jesse akisema suala la mkopo ni jambo la siri kati ya mkopaji na mkopeshwaji na haikutegemewa kwa mtu kama spika kujitokeza hadharani na kutangaza deni la mkopaji.

Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole alisema spika hana mamlaka ya kutangaza deni la mbunge na kama Lema anadaiwa mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni benki aliyoikopa.