Lissu, Spika na mzozo wa mshahara

Muktasari:

  • Hatua hiyo inatokana na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kudai mshahara wake umezuiwa na Bunge kwa muda, huku akisisitiza kuwa yeye bado yupo kwenye matibabu nje ya nchi




Dar es Salaam. Mshahara na posho za kibunge za Tundu Lissu zimeendeleza vuta nikuvute kati ya mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) na uongozi wa Bunge.

Mvutano huo umeibuka baada ya Lissu kudai kuwa stahiki zake hizo za kibunge zimesitishwa na Spika Job Ndugai pamoja na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai tangu Januari huku akiwataka kuzirejesha pasi na masharti yoyote.

Pia, Lissu amewaagiza mawakili wake kuanza mchakato wa kufungua kesi ya madai Mahakama Kuu kutaka arejeshewe stahiki zake zote na kuzuia Bunge kuingilia kwa namna yoyote masilahi yake ya kibunge.

Madai ya Lissu ambaye yupo nje ya nchi tangu aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake Area D, Dodoma ameyatoa juzi kupitia waraka ambao aliusambaza katika mitandao.

Katika waraka huo, Lissu anawatuhumu Spika Ndugai na Kagaigai kusitisha mshahara na posho zake wakati yeye akiendelea na matibabu nchini Ubelgiji jambo ambalo alidai kuwa ni kinyume na Katiba, sheria na taratibu za uendeshaji wa Bunge.

Alipoulizwa jana kuhusu madai hayo, Spika Ndugai alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo mpaka awasiliane na wataalamu wake.

“Tutalifanyia kazi suala hilo. Ili kuwa na jibu la uhakika; lazima ni consult (nishauriane) na watu wangu ili nikisema iwe ni kitu cha uhakika,” alisisitiza Spika Ndugai.

Majibu kama hayo yalitolewa na Kigaigai, “siwezi kuzungumza kitu ambacho sijakiona.”

Katika mkutano wa Bunge uliomalizika mwezi uliopita, Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’ aliomba mwongozo akitaka Bunge lichukue hatua ikiwamo kusitisha mshahara wa Lissu kwani amekuwa akizunguka katika mataifa mbalimbali kuichafua nchini mwongozo ambao Spika Ndugai alisema ataufanyia kazi.

Lissu alisema mshahara na posho za kibunge ambazo kila mbunge hulipwa kila mwezi si fadhila, bali ni haki ya kikatiba na kisheria na kwamba haitegemei utashi binafsi wa Spika wala katibu wa Bunge.

Alizitaja stahili hizo kuwa ni posho ya majukumu kwa ajili ya Spika, Naibu Spika, Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Serikali Bungeni, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wenyeviti wa Bunge na wa Kamati za Kudumu za Bunge. Posho ya jimbo na viti maalumu, msaidizi wa mbunge, dereva na mhudumu.

Alisema Bunge likiwa mhimili wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali, linapaswa kuheshimu sheria, kusimamia haki na taratibu zake na kuzingatia misingi ya haki katika utendaji wa kazi zake.

“Ili kuhakikisha sheria za nchi yetu zinaheshimiwa na haki inatendeka, ninawaelekeza mawakili wangu nchini Tanzania kuanza mchakato wa kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania ili kudai Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai lirejeshe stahili zangu zote zilizozuiwa na kulizuia lisiziingilie na kuziathiri kwa namna nyingine yoyote,” alisema Lissu.