Lissu asema Katiba inakiukwa wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Saturday May 18 2019

Tundu, Lissu ,Lissu , Katiba, inakiukwa ,wakurugenzi, kusimamia, uchaguzi,siasa, chadema, upinzani, ccm,

Tundu Lissu  

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kufuatia mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya jamii kuhusu Mahakama Kuu kufuta sheria iliyowapa wakurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameibuka na kuzungumzia jambo hilo.

Wakati Lissu akieleza hayo Mei 13, 2019  Serikali imekata rufaa Mahakama  ya Rufani kupinga hukumu hiyo.

Katika andiko lake aliloweka katika mitandao ya kijamii leo Jumamosi Mi 18, 2019, Lissu amesema suala la wasimamizi wa uchaguzi ni amri ya Katiba.

“Ibara ya 74(14) ya Katiba inaamrisha kwamba ‘itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa’. Katiba imewataja watu hao 'wanaohusika na uchaguzi' kuwa ni pamoja na "wasimamizi wote wa uchaguzi wa miji na Wilaya zote." (Ibara ya 74(15)(e).”

“Wasimamizi wa uchaguzi hawa ni maofisa wa Tume ya Uchaguzi sio kwa kuteuliwa, bali by operation of the law (kwa utekelezaji wa sheria). Wamelazimishiwa Tume, sio kwa mapenzi ya Tume, bali kwa shuruti ya Sheria ya Uchaguzi,” amesema Lissu.

“Hata hivyo, bado wanabanwa na amri ya ibara ya 74(14) na (15) ya Katiba. Ni marufuku kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa,” amesema Lissu.

Advertisement

Mei 10, 2019 Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Dk. Atuganile Ngwala, Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Pia ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Katika hukumu hiyo mahakama hiyo ilisema kwamba vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao huteuliwa na Rais aliyeko madarakani ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Pia ilisema kwamba sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umetokana na kesi iliyofunguliwa na mashirika kadhaa ya wanaharakati kupitia kwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, akitetewa na Wakili Fatma Karume.

 

Advertisement