Lowassa atakavyoitikisa Arusha kesho

Muktasari:

  • Lowassa ataondoka Dar es Salaam kesho saa tano asubuhi na atawasili Arusha saa sita mchana na kupokewa na viongozi wa CCM ngazi ya mkoa na kisha ataelekea wilayani Monduli atakakopokewa rasmi ndani ya chama na baadaye atafanya mkutano

Dar es Salaam. Wakazi wa Jiji la Arusha na viunga vyake kesho Machi 9, 2019, watampokea aliyekuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa 2015, Edward Lowassa ambaye sasa anaingia mkoani humo akiwa na utambulisho mpya wa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lowassa ambaye ni Waziri mkuu Mstaafu, alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 lakini Machi Mosi, 2019, alirejea rasmi CCM na kuwaambia viongozi na wananchi waliofika kushuhudia kurejea kwake katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam “nimerudi nyumbani.”

Taarifa ambazo Mwananchi imezithibitisha leo, zinasema Lowassa ataondoka Dar es Salaam saa tano asubuhi na kuwasili Arusha saa sita na atapokewa na viongozi wa CCM ngazi ya mkoa na kisha ataelekea wilayani Monduli.

Akiwa Monduli, atapokewa na uongozi wa wilaya na baadaye atahutubia mkutano.

Akizungumza na Mwananchi leo saa tano asubuhi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole amesema baada ya Lowassa kuomba kurejea ndani ya chama hicho Machi Mosi, 2019, alipewa maelekezo kuwa aandike barua kwenye tawi lake ya kuomba kurejea upya.

Polepole anasema tayari Lowassa ametekeleza agizo hilo na vikao husika vimesharidhia kumpokea.

“Kesho ofisi ya CCM Monduli itakuwa na shughuli na vikao na miongoni mwa mambo yatakayofanyika ni kumpokea na kumkabidhi kadi ya CCM,” amesema Polepole.

Alipoulizwa ni viongozi gani wa CCM watakaohudhuria mapokezi hayo, Polepole amesema; “ni tukio la ndani na viongozi watakaohudhuria nitakuambia baadaye.”