Friends of Lowassa waweka msimamo mzito

Muktasari:

Friends of Lowassa na 4U Movement ndio waliokuwa na nguvu kubwa katika mchakato wa Edward Lowassa kuomba kuteuliwa kuwa mgombea Urais 2015 na hatua ya aliyekuwa mratibu wake kugoma kumuunga mkono Lowassa sasa ni gumzo.

 


Moshi. Aliyekuwa mratibu wa kitaifa wa mitandao ya ushindi wa Edward Lowassa mwaka 2015, Hemed Ali amesema kama Lowassa angemshirikisha kabla ya kuhamia tena CCM, angemshauri astaafu siasa.

Ali aliyekuwa mratibu wa makundi mawili yaliyokuwa na nguvu ndani na nje ya CCM mwaka 2015 ya 4U Movement na Friends of Lowassa, amesema pia angemkumbusha namna CCM walivyomtenda 2015.

Mathalan, kundi kama la 4U Movement lilibeba vijana wengi wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu karibu nchi nzima, ambao walipambana kuhakikisha Lowassa anateuliwa na vikao vya CCM.

Katika waraka alioutuma leo Jumanne Machi 5, 2019 kwa wanachama wa Chadema na Watanzania, Ali amesema bahati mbaya sana Lowassa hakumshirikisha katika uamuzi wake huo na tayari amehama na kujiunga CCM.

“Uamuzi huu ni haki yake ya kidemokrasia, hajanihusisha kwa hatua yoyote ile na haikuwa lazima pia kunihusisha lakini laiti angenipa dakika hata moja kabla ya kuhama ningemkumbusha ya 2015,” amesema.

“Ningemkumbusha namna CCM walivyomfanyia 2015, walivyomsimanga, kumvunjia heshima na kebehi kubwa za watu kama ya kaliba ya Polepole, Kibajaji, Msukuma na wengineo,” alisema.

Humphrey Polepole kwa sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wakati Joseph Musukuma ni Mbunge wa Geita Vijijini na Livingstone Lusinde au Kibajaji ni Mbunge wa Mtera, wote kwa CCM

“Pia ningemkumbusha heshima ya Watanzania zaidi ya milioni 6 waliotupa kura ndani ya Chadema kwa kumpigia kura kwa imani kubwa na miongoni mwao wapo tuliosimama pamoja kumpigania,” amesema.

Ali amesisitiza kuwa Lowassa angempa nafasi ya kumshauri, angemshauri asihame kabla ya kushauriana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya kutoka gerezani na ingebidi, angemshauri astaafu siasa.

“Ningemshauri kustaafu siasa kuliko kuhamia CCM jambo ambalo naamini lingekuwa na heshima kubwa kwake lakini kwa masikitiko makubwa haijatokea hivyo na tayari amehamia CCM,” amesema.

Katika waraka wao huo, Ali amewataka wana Chadema na Watanzania wasivunjike moyo au kukata tamaa kwa kuona Lowassa amejiondoa katika kile anachokiamini kuwa ni demokrasia wanayoihubiri.

“Tuendelee kushikamana na kupambana kwa damu na jasho kwani hatua tuliyofikia karibu ukombozi wa Watanzania walio wengi tunaufikia na hizi changamoto zitumike kutuimarisha katika mapambano kuelekea 2020,” amesema.

“Niko tayari kwa lolote na nitasimama kiume kwa mapambano haya. Najisikia fahari kuendelea kuwepo Chadema na hata siku ya kifo changu kinikute nikisimamia misingi ya haki, utu wa watu na demokrasia.”

Ali alibainisha anatambua njia hiyo ya kusimamia haki, utawala wa sheria na demokrasia dhidi ya dola isiyopenda kuona Chadema inasimama imara si rahisi lakini atasimama imara hadi ukombozi upatikane.