Maalim Seif awa namba moja ACT-Wazalendo

Wednesday March 20 2019

Mwanachama namba moja wa ACT Wazalendo, Maalim

Mwanachama namba moja wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) akionyesha kadi yake ya uwanachama baada ya kukabidhiwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar/ Z’bar. Maalim Seif Sharif Hamad, mwamba wa siasa za Zanzibar, ameanza safari mpya ya kisiasa ndani ya chama cha ACT- Wazalendo, akikabidhiwa kadi namba moja.

Ni kadi inayoweza kufananishwa na jezi namba moja inayovaliwa na makipa katika mchezo wa mpira wa miguu, wakiwa na kazi kubwa ya kuhakikisha hakuna mpira unaovuka mstari wa goli.

Safari ya mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) haikuwa peke yake, bali ameambatana na jopo la waliokuwa vigogo wa CUF upande wa Zanzibar na baadhi kutoka Bara.

Safari hiyo ilianza mara baada ya baada Mahakama Kuu kumhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF na kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili tangu Profesa Lipumba abatilishe uamuzi wake wa kujivua uenyekiti wa Agosti mwaka 2015 na kurudi madarakani mwaka 2016.

Shangwe na nderemo zilitawala makao makuu ya chama cha ACT-Wazalendo zilizopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambako katibu huyo mkuu wa zamani wa CUF pamoja na viongozi wenzake wa zamani, walipokuwa wanapokewa rasmi na kukabidhiwa kadi.

Kadi walizokabidhiwa zina namba kati ya moja hadi 22, ambazo wamiliki wake walihama chama na kujiunga na CCM na hivyo kubakia wazi.

Advertisement

Kadi namba moja ilikuwa ya Albert Msendo, aliyekuwa mwanasheria wa chama hicho, lakini alijivua uongozi mwaka juzi kabla ya kutangaza kujiunga CCM.

Zitto alisema kadi hizo zilikuwa za daraja la juu (premium) ambazo nyingi zilinunuliwa na viongozi na kwamba aliyopewa Maalim Seif ambayo iliachwa na Msendo, ilinunuliwa na rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Venance Msebo ambaye alielekeza apewe mwanasiasa huyo wa muda mrefu.

“Ukiwa kiongozi ambaye upo kwenye mioyo za wananchi kamwe hawawezi kukutupa,” alisema Zitto.

Zitto alisema Msebo, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya ACT-Wazalendo amelipa fedha ya kadi Sh500 na malipo ya ada ya miaka kumi, kila mwaka ni Sh1,000.

Alisema uamuzi wao wa kujiunga ACT-Wazalendo ni kuendeleza safari ya kudai demokrasia.

Naye Maalim Seif, ambaye alikuwa amekaa upande wa kushoto wa Zitto katika mkutano huo na akionekana mchangamfu, alisema wameshaachana na CUF, ambayo alishiriki kuianzisha mwanzoni mwa miaka ya 1990.

“Tumepeana talaka na CUF na rasmi leo sisi ni wanachama wa ACT- Wazalendo,” alisema Maalim Seif mara baada ya kupokea kadi ya chama hicho.

Baada ya kuwa kiongozi wa chama na serikalini alikofikia ngazi ya Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais, sasa ni mwanachama wa kawaida, akisubiri mikakati mingine ya ACT Wazalendo.

Kuhusu kadi hizo, Zitto alisema zinatakiwa kukombolewa kwa sababu zilitolewa kwa watu maalumu ambao walikumbwa na dhoruba ya kuhama chama.

Alisema wakati chama hicho kinaanzishwa zilitengenezwa kadi kuanzia namba moja hadi 1,000 ambazo ziliuzwa kwa bei kubwa lakini baada ya baadhi kuamua kutimkia CCM kadi hizo zilikombolewa kisha kupewa wanachama hao wapya.

Katibu wa zamani wa ACT- Wazalendo, Richard Mwigamba alithibitisha suala la kadi hizo kuwa za viongozi.

“Unajua kadi namba moja hadi 20 nyingi zilikuwa za viongozi wa ngazi ya juu ambazo walizilipia fedha nyingi,” alisema Mwigamba, ambaye sasa yuko CCM.

“Kadi yangu ilikuwa namba mbili, lakini kama nimeondoka na amepewa mwingine haina tatizo.”

Wengine waliokuwa na kadi hizo ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliteuliwa kuwa katibu mkuu Wizara ya Maji na sasa amejiunga CCM, hivyo kadi yake kupewa Mansour Yussuf Himid.

Katika shughuli hiyo, Zitto alisema yeye kadi yake ni namba nane na aliichagua hiyo kama heshima kwa aliyekuwa nahodha wa timu ya Liverpool ya Uingereza, Steven Gerrard, huku kadi ya aliyekuwa mkurugenzi wa habari CUF, Salim Bimani atapelekewa kwa kuwa hakuwepo.

Kigogo mwingine, Juma Duni Haji alikabidhiwa kadi namba kumi akisema inaweza kuwa namba ya mchezaji wa Liverpool, Sadio Mane. Duni, ambaye alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Ukawa katika uchaguzi uliopita, pia alimkabidhi Zitto kadi yake ya CUF, akimtaka akampe Profesa Lipumba.

Pia, Nassoro Mazrui aliyepata kadi namba sita na Ismail Jussa amepewa kadi namba 17.

Vigogo wengine

Viongozi wengine waliokuwa CUF ambao jana walikabidhiwa kadi ni Joran Bashange (naibu katibu mkuu), Abubakari Khamis Bakary, Hamadi Masoud Hamadi (wote wajumbe Baraza Kuu) na Kuluthum Mchuchuli (mkurugenzi wa haki za binadamu na sheria), Mbarala Maharagande (naibu mkurugenzi wa habari na uenezi) na Omari Ali Shehe (mkurugenzi wa mipango na uchaguzi).

Wengine ni Mustafa Wandwi (mkurugenzi wa ulinzi na usalama), Bonofasia Mapunda, Najma Khalfan, Zahra Ali Hamadi (wote wajumbe Baraza Kuu) Abdallah Said Khatau (mwenyekiti wa bodi ya wadhamini), Shaweji Mketo (naibu mkurugenzi na uchaguzi), Bwamkubwa Buda (ofisa protokali) na Nurdin Msati (ofisa harakati na matukio). Wengine waliojiunga ni Rehema Shamte Lwambo, Hassan Abdallah Hassan, Asha Msangi na Isihaka Mchinjita.

Advertisement