Maalim Seif azungumzia mvutano wa polisi, ‘CUF Lipumba’

Muktasari:

Leo Jumanne, CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba unafanya mkutano mkuu jijini Dar es Salaam ambapo polisi wa Ilala umeuzuia mkutano huo lakini agizo hilo halikutekelezwa na mkutano uliendelea

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameifananisha vuta nikuvute inayoendelea kati ya polisi na viongozi wa chama hicho upande wa Profesa Ibrahim Lipumba kama mchezo wa kuigiza kwa jambo ambalo lipo wazi kuwa mkutano huo si halali.

Amesema jeshi la polisi likiamua lina uwezo mkubwa wa kuzuia mkutano huo unaoendelea jijini Dar es Salaam kutokana na zuio la mahakama lilitolewa kuhusu mchakato huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 12, 2019, Maalim Seif amesema “Ni kama mchezo wa kuigiza kuhusu suala hili.”

“Kama polisi ina nia ya dhati ya kuzuia wale hawawezi kufanya lolote lile. Utafanyaje mkutano wakati kuna zuio tena la Mahakama Kuu? Amehoji Maalim Seif.

“Siyo mantiki yoyote kwa polisi kuanza kuzungumza na viongozi wa CUF wa upande ule wakati suala lipo wazi kabisa. Nawaambia msimamo wetu upo pale pale mkutano huu hatuutambui kabisa kwa sababu ni haramu,” amesema Maalim Seif.

Hata hivyo, Profesa Lipumba amesitisha kwa muda mkutano hadi saa tisa alasiri utakapoendelea tena, ikiwa ni baada ya polisi kurejea ukumbini hapo na kuuzuia kwa mara nyingine.