Mabilionea 26 wamiliki uchumi sawa na nusu ya maskini duniani

Muktasari:

Shirika la kimataifa la Oxfam limebainisha katika ripoti yake kwamba matajiri wachache wanamiliki utajiri kuliko utajiri unaomilikiwa na nusu ya watu masikini duniani. Oxfam imezitaka Serikali duniani kuwatoza kodi kubwa matajiri ili kupunguza pengo kubwa lililopo baina yao.

Nairobi, Kenya. Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kimataifa la Oxfam inaonyesha kuwa mabilionea 26 duniani wanamiliki utajiri ulio sawa na nusu ya watu maskini zaidi duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya DW, Oxfam imezitaka Serikali kuongeza kodi kwa matajiri ili kupunguza pengo la kukosekana usawa. Ripoti hiyo imetolewa leo Januari 21 mjini Nairobi, kuelekea kongamano la kimataifa la kila mwaka la kiuchumi litakalofanyika mjini Davos Uswisi.

Ripoti imebainisha kuwa mabilionea duniani wameshuhudia utajiri wao ukikua kwa dola bilioni 2.5 kwa siku mwaka 2018. Watu bilioni 3.8 walio chini ya kiwango, utajiri wao ulishuka kwa asilimia 11 mwaka jana, kwa mujibu wa Oxfam.

Shirika hilo limesisitiza kuwa ongezeko la pengo baina ya matajiri na maskini, na kwamba linazuia mapambano dhidi ya umaskini, kuharibu uchumi na kuchochea hasira ya umma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Oxfam, Winnie Byanyima amenukuliwa akisema Serikali zimepunguza kodi kwa mashirika makubwa katika muongo mmoja uliopita.

Amesema kushindwa kufanya hivyo, wanahamisha mzigo wa kodi kwa wananchi hasa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat).

“Kodi zisizo za moja kwa moja ambazo zinatozwa kwenye chumvi, sukari na sabuni; mahitaji muhimu ya wananchi… maana yake ni kwamba wananchi wanalipa zaidi kwa vipato vyao ukilinganisha na matajiri,” amesema Byanyima akinukuliwa na Reuters.