Magufuli afanya ziara ujenzi wa daraja la Selander

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mhandisi Mshauri wa kampuni ya Yoosin Engineering Mhandisi Suk-Joo Lee wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa daraja linalokatiza baharini na kuunganisha maeneo ya Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam. Daraja hilo limependekezwa kuitwa Tanzanite Bridge.

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la Selander jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la Selander jijini Dar es Salaam ambapo amefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wake.

Daraja hhilo litaakalopita baharini kuanzia ufukwe wa Coco Beach (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road), Jijini Dar es Salaam linatarajiwa kukamilika Oktoba 2021.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Juni 24, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais Magufuli amekutana na mhandisi mshauri wa Kampuni ya Yooshin Engineering, Suk-Joo Lee aliyemwelezea mkandarasi huyo kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo linalotarajiwa kupunguza msongamano wa magari kutoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya GS Engineering ya Korea, Suk-Joo Lee anakamilisha kuunganisha daraja la muda litakalomwezesha kuanza ujenzi wa nguzo za daraja. Kwa ujumla kazi imefikia asilimia 10.12,” amesema Rais Magufuli

Suk-Joo Lee amesema amefurahishwa na mazingira ya kufanya kazi Tanzania, akiahidi kazi hiyo itakwenda vizuri.

Katika taarifa hiyo imeeleza daraja hilo lililopendekezwa kuitwa Tanzanite Bridge  litakamilika Oktoba 2021, likiwa na urefu wa kilometa 1.03 pamoja na barabara za kuunganisha zenye urefu wa kilometa 6.23.

Taarifa hiyo imesema utekelezaji wa mradi huo unahusisha ujenzi wa nguzo za msingi zenye urefu wa kati ya meta 14 na 65 na utagharimu takribani Sh255 bilioni.