Magufuli amuapisha Dk Ulisubisya, mabilioni yatengwa miradi ya kilimo Tanzania

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada wakati wa hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu Mei 20, 2019.

Muktasari:

Dk Mpoki Ulisubisya,  leo Jumatatu Mei 20, 2019 ameapishwa na Rais John Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kuchukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyevuliwa ubalozi

Dar es Salaam. Dk Mpoki Ulisubisya,  leo Jumatatu Mei 20, 2019 ameapishwa na Rais John Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kuchukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyevuliwa ubalozi.

Novemba, 2018 Rais Magufuli alimrejesha nchini Kidata na kumvua hadhi ya ubalozi bila kueleza sababu za kufanya hivyo.

Dk Ulisubisya aliyeteuliwa kuwa balozi Janauri 9, 2019 ameapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wengine waliohudhuria ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kabla ya uteuzi huo Dk Ulisubisya alikuwa katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia afya na nafasi yake ilichukuliwa na Dk Zainabu Chaula.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden, Peter Eriksson.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa leo inaeleza kuwa amempongeza Magufuli  kwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ameeleza dhamira ya Sweden kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umetenga Sh127.3 bilioni kwa ajili ya kufadhili miradi ya kilimo nchini kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia mwaka 2020.

Rais wa IFAD, Gilbert Houngbo amesema baada ya kutenga fedha hizo, IFAD inasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo mahsusi ya miradi ya kilimo ambako fedha zitaelekezwa.

Rais Magufuli ameishukuru IFAD kwa ushirikiano wake na Tanzania na alimhakikishia Houngbo kuwa ushirikiano na uhusiano huo ulioanza mwaka 1978 utadumishwa kwa maslahi ya Watanzania.

Amesema fedha zilizotengwa katika mpango huo wa miaka mitatu zitaelekezwa katika maeneo yenye maslahi mapana ya sekta ya kilimo ikiwemo kuwezesha matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji na kuzalisha mbegu bora za mazao.

Pia, zitatumika kutatua changamoto ya masoko ya mazao, kuboresha ufugaji na ameipongeza IFAD kwa kutoa fedha pasipo kuweka masharti ya maeneo zinakopaswa kuelekezwa.

Hata hivyo Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuharakisha mchakato wa kuainisha maeneo yatakayopokea fedha hizo ili utekelezaji wa mpango huo uanze.