Mahakama yaibana Serikali upelelezi kesi yakina Mwanyika

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kueleza hatua waliyofikia katika upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Rais wa migodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu, Deo Mwanyika (56) na wenzake sita.

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kueleza hatua waliyofikia katika upelelezi wa kesi nya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Rais wa migodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu, Deo Mwanyika (56) na wenzake sita.

Mwanyika na mwenzake wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwamo ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi.

Maelekezo hayo yametolewa leo Aprili 23 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa wanasubiri majibu kutoka nje ya nchi ili kukamilisha upelelezi huo.

Hakimu Mhina amesema pamoja na kwamba upande wa mashtaka wako katika hatua ya ufuatiliaji lakini wanatakiwa wafikie hatua muhimu ya kueleza walikofikia katika upelelezi wao.

" Upande wa mashtaka pamoja na kuwa mpo katika hatua ya ufuatiliaji wa majibu nje ya nchi lakini mnatakiwa mfike hatua muhimu ya kueleza mlikofikia juu ya upelelezi wenu kuliko kusema tu upelelezi bado haujakamilika," amesema.

Hakimu Mhina baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 3, 2019 itakapotajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kutokana na shauri hilo kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Awali, wakili wa Serikali, Wankyo Simon alieleza kuwa kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo leo kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika kwani bado wanasubiri majibu kutoka nchi za nje.

“Bado tunaendelea kusubiri majibu kutoka nchi za nje ili tuweze kukamilisha upelelezi wetu, hivyo tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa," alisema Simon.

Mbali na Mwanyika , washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 77/2018 ni meneja mahusiano wa mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo;  mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo, kampuni ya mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration Du Nord LTEE na Bulyanhulu.

Kati ya mashtaka 39 yanayowakabili;  17 ni ya utakatishaji fedha; nane ya ukwepaji kodi; saba ya kughushi nyaraka; matatu ya kula njama na moja moja la  kusaidia kuongoza uhalifu, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutoa rushwa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Aprili 11, mwaka jana na Juni 30, 2017 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,  Kahama, Tarime na Biharamulo pamoja na maeneo mbalimbali ya mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini, Toronto nchini Canada, visiwa vya Barbados na nchini Uingereza, walikula njama ya kutenda makosa hayo.

Katika shtaka la kutoa rushwa, Mwanyika na Lugendo, wanadaiwa kutoa rushwa ya Sh 718 milioni kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga, Hussein Kashindye kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya kijinai yaliyokuwa yametendwa na mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kukwepa kodi, inadaiwa kati ya Mei 16, mwaka jana na Desemba 31, mwaka jana katika maeneo hayo wakiwa na nia dhahiri, walitoa tamko la uongo kwa kamishna mkuu wa (TRA kwa lengo la kukwepa kodi ya dola za Marekani 9 milioni.