Majaliwa atoa ahadi mpya ya malipo ya korosho

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameahidi kumalizia malipo ya korosho ya msimu wa mwaka 2018 ndani ya mwaka huu wa fedha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wakulima wa korosho ambao  hawajalipwa kuwa Serikali italipa fedha hizo ambazo ni zaidi ya Sh20 bilioni mwaka huu.

Majaliwa amesema wakulima ambao hawajalipwa au kumaliziwa malipo yao baada ya Serikali kumaliza uhakiki majina yao yatapelekwa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa ajili ya malipo.

Taarifa ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jumamosi, Juni mosi 2019,  imesema Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Lindi, kilichofanyika kwenye ukumbi wa CCM mkoa.

“Wakulima wote wanaodai malipo yao ya korosho watalipwa katika mwaka huu wa fedha kwa kuwa ni haki yao na Serikali haitodhulumu haki ya mkulima yeyote,” amenukuliwa Majaliwa.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema ulipaji wa korosho unaendelea.

Zambi amesema hadi Mei 31 mwaka huu zaidi ya kilo milioni 51.99 zenye thamani ya zaidi Sh171.57 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 87.6 zimeshalipwa kwa wakulima husika.

Mkuu huyo wa mkoa amesema Sh23.4 bilioni hazijalipwa kwa wakulima wa korosho wa mkoa huo na kwamba, zilihakikiwa kituo cha Mtwara.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wabunge wa Mkoa wa Lindi, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na manispaa pamoja na wakuu wa idara.