Majaliwa atoa neno wizi wa mitihani, viboko shuleni

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya maofisa elimu nchini wanaoshirikiana na walimu kujihusisha na wizi wa mitihani huku akikemea tabia ya walimu kuchapa viboko wanafunzi bila kufuata utaratibu

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya maofisa elimu wa mikoa na wilaya wanaoshirikiana na walimu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani akiwataka kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa inalivunjia heshima Taifa.

“Kamati za mitihani za mikoa na wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na utumishi kwa mujibu wa sheria. Hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa,” amesema Majaliwa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Machi 26, 2019 katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa sita wa umoja wa maofisa elimu wa wilaya (Redeoa) uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) ni chombo kilichojijengea sifa kwa muda mrefu barani Afrika, kwamba Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha rasilimali ili kukifanya chombo hicho kuwa imara na cha kisasa. 

Amebainisha kwa hali hiyo imezifanya nchi mbalimbali kuja Tanzania kujifunza masuala ya upimaji na uendeshaji wa mitihani.

“Nimejulishwa pia hivi sasa hapa nchini wapo viongozi wa mabaraza ya mitihani kutoka nchi za Afrika Mashariki,” amesema.

Waziri Mkuu pia amezungumzia nidhamu mbaya ya wanafunzi akibainisha hilo ni jukumu la walimu wote, akiwataka kutekeleza majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuongoza na kuwaendeleza.

Viboko shuleni

Kuhusu viboko shuleni, Majaliwa amesikitishwa na jambo hilo likiwemo tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera. 

“Ninatambua si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni,” amesema Majaliwa.

“Maofisa elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni zake.”

Ameongeza, “Adhabu ya viboko itatolewa iwapo kutatokea  utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Na adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina hakika tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma.”